Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi
mema, kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, kuwasaidia wagonjwa, maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, lakini kwa namna ya pekee kabisa kuwaonjesha huruma
na mapendo, wagonjwa walioko kufani! Hiki ndicho kielelezo makini cha huruma na upendo
unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Canada linabainisha kwamba, kumsaidia mgonjwa kupata kifo laini si tendo na huruma,
haki wala uungwana bali ni mauaji ya kikatili, kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka
kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na kuheshimiwa na wote. Hukumu iliyotolewa
na Mahakama kuu ya Canada hivi karibuni kwamba, madaktari wanaweza kuwasaidia wagonjwa
walioko kufani au wenye magonjwa yasiyokuwa na tiba kupata kifo laini, ni hukumu inayokwenda
kinyume na utu na haki msingi za binadamu, kwani kila mtu anayo haki ya kuishi.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasaidia
na kuwafariji wagonjwa, ili asiwepo kamwe mgonjwa ambaye atakumbwa na upweke kiasi
hata cha kujikatia tamaa ya maisha na kutamani kupata kifo laini. Baraza la Maaskofu
kwa upande wake, litaendelea kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu msingi pamoja na
kuwasaidia wagonjwa wa walioko majumbani; wazee na walemavu, ili kuonja huruma na
upendo wa Mungu.
Maaskofu wanaishauri Serikali kufuta hukumu hii inayoonekana
kuwa na huruma kwa wagonjwa lakini ndani mwake, inafumbata utamaduni wa kifo, changamoto
kwa viongozi wa Serikali kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma bora na makini kwa wananchi
wao; wanawataka mawakala wa Serikali na wanataaluma kuibua sera na mikakati inayoheshimu
uhuru wa dhamiri kwa wafanyakazi wote na kwamba, mauaji hayawezi kukubalika kwa kisingizio
cha huruma kwa wagonjwa dhidi ya mateso na mahangaiko yao.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.