2015-02-11 15:59:10

Wambeya hawana Bunge!


Hapa duniani kuna aina ya magonjwa mabaya sana, sugu na ya kuambukiza. Wanaoumwa magonjwa hayo wanaogopwa na kutengwa hadi na jamii zao. Ishi ya wagonjwa hao inakuwa ya kuomba yala maskini na kutegemea kudra ya Mungu. Mbaya zaidi watu wanaojidai kuwa na maadili mema ikiwa ni pamoja na watu wa dini wataisadikisha jamii kwamba magonjwa hayo yamesabishwa na dhambi na hivi Mungu amewaadhibu wagonjwa au jamii yenye ugonjwa huo kutokana na uvunjaji wa maadili. Pahala pengine hata serikali ya nchi inaridhia kutengwa kwa wagonjwa hao na kuwanyima huduma muhimu za maisha.


Fikra hizo zaweza kuwaaminisha na kuwavunjisha moyo hata wagonjwa mwenyewe hadi wakajisikia kuwa wamelaaniwa na Mungu. Hivi ndivyo yanavyoonwa magonjwa ya ukimwi, ebola, Kifua kikuu, ulemavu wa ngozi, ukoma nk. Magonjwa hayo balaa yanayosabisha mtu kuchukiwa na kutengwa na jamii, hata mwenyewe kujishuku kuwa ni laana ya Mungu. Magonjwa hayo tunaweza kulinganishwa pia na ujambazi, uuaji, hata gonjwa la rushwa, siasa kali ya dini, hivyo huchukiwa hata na mataifa mengine kiasi yaweza yakaeleweka kuwa kama ni laana ya Mungu. Ndiyo maana mtoto mwizi anaweza kuambiwa: “mtoto huyu ni laana mtupu.”

Leo tunakutana na mganga na mwanamapinduzi anayetaka kutuonesha kwamba wagonjwa hao ni binadamu sawa kama wengine, isipokuwa kwa bahati mbaya ni ugonjwa tu ndiyo uliowanyima hadhi ya kuwa na utu wa kuwa katika jamii, hadi waishie ombaomba, au kutengwa na jamii, aidha, ugonjwa huo siyo laana ya Mungu.

Ndugu zangu, mwanzoni mwa safari ya Yesu tumepambana na vituko viwili vya kimapinduzi alivyoisha vifanya. Mosi, kule kwenye Sinagogi anapomrudishia mtu uhuru wa utu wake uliokuwa umekaliwa na mapepo. Pili, anaiponya homa ya ubinafsi iliyomnyima mkwe wa Petro uhuru wa kutumia utu wa upendo ili aweze kutumikia. Kituko cha leo kinafuatia baada ya Yesu kutoka kusali ili kuhusianisha matendo yake na upendo wa Mungu, kusudi aweze kuona mambo vizuri kwa jicho la Mungu anayewapenda watu wote. Baada ya kusali anaona watu wote ni waana wa Mungu wanaohitaji upendo wake.

Mapato yake Yesu anaporudi tu toka kusali anakutana na mkoma, tunaambiwa: “Akaja kwake mtu mwenye ukoma.” Mgonjwa huyo amekataliwa na wote, hana uhakika pengine hata Mungu amemlaani kama alivyoaminishwa na sheria ya mahakama ya dini iliyosema: “Mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitatuliwe, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, ‘Ni najisi! Ni najisi!’ Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake, makazi yake yatakuwa nje ya marago.” (Walawi 13:45-46).

Kwa hiyo mkoma hakuweza hata kukaribia hekaluni kusali na wengine, na yeyote ambaye angethubutu kumkaribia na kumgusa mkoma naye alihesabiwa kuwa mdhambi na chukizo kwa Mungu. Ndiyo maana, Naamani mkoma generali wa Asiria toka Damaso anaenda kwa nabii Eliseo kwa vile alisikia kuwa ni mganga anayeponya ukoma. Anapofika kwa Eliseo, nabii anaogopa kumpokea anajitenga naye kabisa, badala yake anamtuma mtumishi wake akaonane na Naamani na amwambie aende kuoga kwenye mto Yordani mara saba.

Kitu cha kushangaza kwa Mkoma anayetajwa katika Injili ya leo, hana jina wala sura ila inasemwa tu: “Akaja kwake mtu mwenye ukoma.” Mkoma huyu anatambua kwamba Yesu ni mtu pekee anayeweza kumrudishia utu wake. Anaamini kwamba Injili ya upendo aliyoileta Yesu inaweza kumponya. Hivi anajitosa kumwendea Yesu anampigia magoti na kumsihi “Kama ukitaka waweza kunitakasa,” ni sawa na kumhoji Yesu: Je, unataka kuafiki kile wanachosema watu wote, walawi, makuhani, walionitenga au mapolisi walionishika, inavyosema serikali na zinavyoamini dini zote? Je, upi ni msimamo wa Mungu kutokana na hali ya ugonjwa, ya machungu, ya kutengwa na jamii unayoniona nayo?

Yesu akiwa mwana mapinduzi anayetaka kuingiza sera mpya duniani, mbele ya hali hii ya mtu aliyeachwa na wote, Yesu ananywea kabisa yaani anavutwa na huruma, kama inavyosemwa: “Naye akamhurumia.” Hapa unaona fikra za Mungu ni kuonea huruma, anao upendo mkuu kwa binadamu. Hali hiyo ni ya mapinduzi makubwa sana anayofanya Mungu dhidi ya fikra za binadamu.

Kisha Yesu “ananyosha mkono wake.” Hapa unapata picha ya Agano la Kale pale Mungu anaponyosha mkono kule Misri kwa Farao na ikaja adhabu ya kuangamiza uovu, ili kumpa mtu uhuru wake. Kadhalika Yesu ananyosha mkono ili kuuadhibu uovu yaani ukoma. Ananyosha mkono kwa upendo anamgusa na kumjibu mkoma mara moja: “Nataka takasasika” Mara moja mkoma anaponywa. Kwa Lazaro alisema pia “Ndiyo nataka, toka nje” (Yoh 11:43) Kwa binti Yairusi alisema pia, “Talika kumi, Nataka inuka” (Mk. 5:41). Hapa unalishuhudia tena nguvu ya Neno linavyoponya.

Sehemu ya pili ya Injili ni ngumu kuielewa inaposema: “Akamkataza kwa nguvu, akamwambia “Angalia usimwambie mtu neno lolote, ila enenda ukajioneshe kwa kuhani ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwako.” Kukataza kwa nguvu, kwa kigiriki ni EmbrimEsamenos maana yake kumgombeza kwa nguvu sana, kisha akamwondoa mara, kwa kigiriki ni Exebalen ni kama kumwambia: “toka hapa!” Yesu amembadilikia mgonjwa kwa ghafla. Kulikoni Yesu amfanyie hivi mtu ambaye mwanzoni alionekana kumwonea huruma, kumpenda na kumponya sasa anampa maonyo makali na kumfukuza? Ukweli ni kwamba mkoma huyu alipomjia Yesu hakutokea nyumbani kwake, bali alitokea nje utengoni kwa wakoma wenzake.

Hapa mkoma anawakilisha watu wote, au fikra za binadamu wote kijumla zinazowatenga wenye ukimwi, wakoma na wadhambi kuwa wamechukiwa pia na Mungu. Yesu sasa anataka kufukuzia mbali mawazo na fikra hizo potovu. Mbele ya Mungu wewe hujalaaniwa wala kutengwa. Ndiyo maana anamgombeza na kumkanya “Achana kabisa na fikra hizo. Fikra namna hiyo ni ugonjwa wa kuutoroka kama ulivyo ukoma.”

Kisha akamwagiza tena “usimwambie mtu yeyote.” Kwa hoja kwamba kumponya mkoma ni kama kumfufua mfu. Manabii walisema kwamba wakati mwafaka afikapo masiha, huyo angeponya wakoma, hivi Yesu hakutaka kujulikana hivyo toka mwanzo kwani angeleta mtafakaruku na sintofahamu. Yesu alitaka ajioneshe mwenyewe waziwazi kuwa ni masiha pale atakapojitoa maisha yake msalabani kwa ajili ya watu.

Hivi anamwambia tu “enenda ukajioneshe kwa kuhani ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwako,” yaani aende kushuhudia kwao kwamba amefika mtu anayewapokea na kuwagusa wakoma. Kwamba mungu wanayemtangaza wao si wa kweli.

Mkoma alipoondoka anafanya kinyume cha alivyokatazwa: “Akaanza kulitangaza Neno lile.” Kutangaza hapa kigiriki ni ton logon (logon ni neno, ujumbe) yaani “kuhubiri maneno mengi” Kama vile Yesu angemtuma kwa kutumia usemi wa mitaani “Kantangaze.” Mtu aliyekuwa ametengwa sasa amekuwa katekista, na mtangazaji wa Injili au habari njema aliyotendewa, kwamba Mungu anawapenda watu wote na siyo kama alivyokuwa amehubiriwa kabla. Hayo ndiyo mapinduzi mengine mapya, kwamba mtu huyo sasa anatanga mang’amuzi aliyotendewa na Mungu.

Mapato yake tunasikia kwamba: “Yesu hakuweza tena kuingia mjini kwa wazi, bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wa wagonjwa wakamwendea kutoka kila mahali”. Ona tena hapa uzuri wa mganga na mwanamapinduzi huyu. Kwamba mwanzoni mkoma alizuiwa kuingia mjini sababu ya ugonjwa wake, akatengwa na jamii yake na akaenda kukaa nje pahala pasipokuwa na watu isipokuwa wagonjwa wenzake wa ukoma. Sasa amepona anaingizana mjini. Mambo yamebadilika, ni sawa kama mkoma yule angemwambia Yesu, “kutesa kwa zamu.” Sasa ni zamu ya Yesu anaenda kukaa nje utengoni mahali kusiko na watu isipokuwa wagonjwa waliotengwa ndiyo wanaomwendea.

Hata sisi tunaweza kujisikia kutengwa na jamii kutokana na magonjwa yetu, hasahasa tabia zetu mbovu. Tunahimizwa kujitambua hali ya ukoma iliyo ndani mwetu, na tumwendee Yesu ambaye hakai mjini kwa watu wazima bali yuko na sisi watengwa, watu waovu ingawaje yeye si mkoma au mwovu. Yuko tayari kutuponya na kutuingiza tena katika jamii. Huu ndiyo upendo wa Mungu. Huu ndiye mganga na mwanamapinduzi. Haya Kanitangaze!

Fadre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.