Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Vatican inaendelea
kufuatilia kwa umaskini mkubwa machafuko na vita inayoendelea sehemu mbali mbali za
dunia na kati yake ni vita huko Ukraine, ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa
kwa watu na mali zao. Mara kadhaa, Baba Mtakatifu Francisko amewasihi wadau mbali
mbali kusitisha vita na kuanza kujikita katika majadiliano ya kisiasa ili amani iweze
kupatikana, lakini hadi sasa juhudi hizi zote zimegonga mwamba.
Baba Mtakatifu
anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea
watu waliofariki dunia kutokana na vita huko Ukraine pamoja na wale ambao wamepata
majeraha ili waweze kupona haraka. Jambo la msingi ni majadiliano, ili kweli amani
iweze kupatikana badala ya kuendelea na mtindo wa sasa wa kulaumiana na kushambuliana.
Majadiliano ya kisiasa pamoja na kuzingatia sheria za kimataifa ni mambo msingi yanayoweza
kusaidia mchakato wa amani ya kudumu nchini Ukraine.
Hapa kama alivyowahi
kusema Mtakatifu Yohane Paulo II kuna haja kwa binadamu kuwa na ujasiri wa kutumia
hoja ya nguvu kwa kujikita katika hoja ya sheria. Baba Mtakatifu anasubiri kwa hamu
na matumaini makubwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ukraine
wakati wa hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican.
Maaskofu hawa watakuwa mjini Vatican kuanzia tarehe 16 hadi 21 Februari 2015.
Hapa itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kupata habari za moja kwa moja kwa kile kinachoendelea
nchini Ukraine, tayari kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho.
Baba Mtakatifu
Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Chancellor, Angela Merkel mjini Vatican
tarehe 21 Februari 2015. Mgogoro wa Ukraine ni kati ya ajenda ambazo, bila shaka Baba
Mtakatifu atapenda kuzungumza na mgeni wake, ili kuonesha wasi wasi wake kuhusiana
na hali halisi huko Ukraine.