Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji
kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, katika maadhimisho ya Siku ya ishirini na tatu
ya wagonjwa duniani kwa mwaka 2015 anasema, kuna uhusiano mkubwa kati mgonjwa, mhudumu
na jamaa kwani wote kwa pamoja wanafanya hija ya maisha inayojikita katika hekima
ya moyo. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu "Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu
kwa aliyechechemea".
Mahusiano kati ya mgonjwa na mhudumu wa afya ni mkutano
ambao unajenga na kuimarisha imani ambayo mgonjwa anaijenga kwa daktari na utambuzi
ambao daktari anaudhihirisha kwa mgonjwa kutokana na taaluma yake na kwamba, Kanisa
hapa linatambua kuwa hii ni huduma inayolenga kudumisha Injili ya Uhai. Tiba pamoja
na mambo mengine haina budi kuzingatia maisha ya mtu: kimwili, kiroho na kisaikolojia,
hapa hekima ya moyoni haina budi kuzingatiwa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.
Wahudumu
wa sekta ya afya wawaone wagonjwa kuwa kama ndugu zao, ili kweli huduma wanayoitoa
iwe ni ushuhuda wa faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mahali pa kutangaza uwepo wa
Ufalme wa Mungu. Huduma kwa wagonjwa ni hija ya kuutafuta utakatifu wa maisha; fursa
ya kukuza na kuimarisha imani, matumaini na mapendo sanjari na kutangaza Injili ya
Uhai, kwa njia ya huduma makini. Wahudumu wa sekta ya afya wanaalikwa kuwa kweli ni
Wasamaria wema wanaowaganga wagonjwa kwa mafuta ya upendo na huruma inayobubujika
kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni
wa upendo na mshikamano wa kidugu katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa
na mahangaiko ya watu; kwa kutambua kwamba, kila tendo wanalolitenda kwa ajili ya
wagonjwa wanamtendea Kristo anayejifananisha na watu kama hawa. Wagonjwa na wote wanaoteseka:
kiroho na kimwili ni hazina kubwa katika maisha na utume wa Kanisa; wanayo heshima
na utu wao kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Wagonjwa waonjeshwe,
urafiki na udugu wa kweli bila kuwakejeli wala kuwadhihaki. Mgonjwa ana hamu ya maisha
na anashiriki kikamilifu katika asili ya mwanadamu na kwamba, anahitaji kuonjeshwa
upendo na huruma; mambo ambayo yanajikita anasema Monsinyo Mupendawatu katika toba
na wongofu wa ndani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.