Mheshimiwa Padre Ernest Ngboko Ngombe ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lisala,
DRC
Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Louis Nkinga
Bondala wa Jimbo Katoliki la Lisala lililoko nchini DRC ili kung'atuka kutoka madarakani.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Ernest Ngboko Ngombe, C.I.C.M,
Makamu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Scheut kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki
la Lisala.
Askofu mteule Ernest Ngboko Ngombe alizaiwa tarehe 25 Mei 1964
Jimboni Lisala baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa nchini Cameroon, aliweka
nadhiri zake za kwanza kwenye Shirika hapo tarehe 17 Oktoba 1987 na baadaye kupadrishwa
tarehe 20 Juni 1996 huko Dakar, Senegal.
Tangu wakati huo katika maisha na
utume wake kama Padre amekuwa Paroko msaidizi, Mkuu wa Shirika mahalia na kuanzia
mwaka 2001 hadi mwaka 2011 alipelekwa kujiendeleza kwa masomo ya juu katika masuala
ya kitaalimungu na kujipatia Shahada ya Uzamili kutoka katika Chuo Kikuu cha Catholic
Theological Union, kilichoko nchini Marekani.
Kunako mwaka 2011 aliteuliwa
kuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya Kitaalimungu iliyoko nchini Cameroon na Mratibu
wa Shirika, Kanda ya Afrika. Kunako mwaka 2011 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya
wa Jimbo Katoliki Lisala, amekuwa ni Makamu mkuu wa Shirika na makazi yake yakiwa
mjini Roma.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.