2015-02-11 08:43:45

Jicho la matumaini Barani Afrika!


Kardinali mteule Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA anasema kwamba, Wakatoliki nchini Ethiopia ni kundi dogo, lakini ambalo limeendelea kutoa mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ethiopia, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu na mafao ya wengi.

Kuna mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume ambayo yanaendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa Katoliki linaendelea kukua na kupanuka kwa idadi ya waamini pamoja na maboresho ya huduma msingi; hapa hakuna mashindano ya kunyang'anyana waamini na Kanisa la Kiorthodox kwani majadiliano ya kiekumene yanajikita katika uhalisia wa maisha na huduma. Changamoto kubwa kwa Wakristo ni kujishikamanisha na Kanisa zaidi kwa kuondokana na uwili katika maisha; mambo ambayo yanawafanya kukumbatia: imani, mila na tamaduni ambazo zinasigana kimsingi na Injili ya Kristo.

Kardinali mteule Souraphiel anabainisha kwamba, Wamissionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika Afrika kwa ajili ya Uinjilishaji, wamechangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika katika medani mbali mbali za maisha. Wamissionari hawa wengi wao wamefariki dunia kutokana na kushambuliwa na Malaria, lakini huduma yao bado inahifadhiwa kwenye sakafu ya mioyo ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

Nchi nyingi Barani Afrika zinaendelea kuadhimisha Jubilee ya miaka mia moja ya Uinjilishaji katika maeneo yao. Kwa bahati mbaya, Ethiopia haikufanikiwa kujifungua mapema zaidi kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji, vinginevyo, ingeweza kuwa ni kati ya wadau wakuu wa Uinjilishaji Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.