Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Jumanne tarehe 10 Februari
2015 katika Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, iliyoongozwa na Askofu mkuu Savio
Hon Tai-Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amekiri Kanuni
ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Kanisa anapotekeleza dhamana na wajibu wake wa
kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huku akiwa ameungana na Maaskofu
wenzake.
Ibada hii
imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata na Rais wa
Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa pamoja na baadhi ya Watu wa Familia ya Mungu kutoka
Tanzania. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mwenyeheri Kardinali Newman
kilichoko kwenye Makao Makuu ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, mahali ambapo
kwa kawaida Maaskofu wateule wanakiri na kula kiapo cha utii kwa Kanisa.
Katika
kiapo cha utii, Askofu mteule Sangu ameahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano
wa Kanisa; kulinda amana ya Mafundisho ya Kanisa na kuwasaidia wale wote wanaokengeuka
kuufahamu ukweli wa imani ya Kanisa Katoliki. Atajitahidi kuwa ni Mchungaji mwema,
akifuata mfano wa Yesu Kristo Kuhani mkuu. Atasimamia nidhamu kadiri ya Sheria za
Kanisa na Kanuni katika maadhimisho ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.
Askofu
mteule Sangu ameapa kwamba, atasimamia mali ya Kanisa kwa uaminifu na kuonesha upendo
na mshikamano wa pekee na Mapadre pamoja na Mashemasi ambao ni wasaidizi wake wa karibu
na kwamba, atajitahidi kukuza na kuendeleza miito mitakatifu ndani ya Kanisa; pamoja
na kuhamasisha ari na moyo wa shughuli za kimissionari zinazotekelezwa na Watawa mbali
mbali Jimboni mwake. Mwishoni, atawajibika kwa Baba Mtakatifu na Baraza la Maaskofu
Katoliki katika utekelezaji wa majukumu yake kadiri ya Sheria za Kanisa.