Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amelisifu
Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) duniani kwa kujali na kushughulikia matatizo
ya vijana akisema kuwa vijana wa kizazi kipya wanapitia katika dunia ngumu zaidi na
majaribu makubwa zaidi kuliko marika yaliyowatangulia.
“Nimefurahi na nawapongeza
kuwa pia mliangalia matatizo ya vijana katika mkutano wetu wa Dar es salaam kwa sababu
vijana wetu wanapitia katika dunia ngumu zaidi na majaribu makubwa zaidi kuliko yale
ambayo sisi wazazi wao tulipitia,” Rais Kikwete aliuambia uongozi wa SDA ukiongozwa
na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo duniani, Dkt. Ted N.C. Wilson na kuongeza: “Vijana
wetu sasa wanakabiliwa na mifumo ya kisasa zaidi ya mawasiliano duniani ambayo inawalazimisha
kukabiliana na majaribu mengi – televisheni imekuwa ya dunia nzima (global), intaneti
sasa imekuwa ya dunia nzima na mitandao ya mawasiliano ya kijamii imekuwa ya dunia
nzima na kila kimoja kinashusha aina yake ya habari kwa vijana wetu.”
Pongezi
hizo kwa SDA zilitolewa mwishoni mwa wiki, Jumamosi, Februari 7, 2015, na Rais Kikwete
wakati wa chakula cha jioni ambacho aliwaandalia viongozi hao wa SDA kutoka sehemu
mbali mbali duniani, zikiwemo nchi 11 za Afrika, wakiongozwa na Dkt. Wilson ambaye
ni Kiongozi Mkuu wa SDA na Rais wa the General Conference of the Seventh Adventist
Church.
Dkt. Wilson na viongozi wa SDA kutoka nchi mbali mbali duniani walikuwa
nchini kushiriki katika mkutano wa kidini ujulikanao kama Blessings in Mission East
and Central Africa ambao ulifanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar Es Salaam.
Dkt. Wilson alimweleza Rais Kikwete kuwa Kanisa lake limefanya mkutano mzuri na wa
kuvutia na kuwa inakadiriwa kuwa kiasi cha watu 40,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania
walishiriki mkutano huo.