2015-02-10 08:42:10

Iweni ni mashuhuda wa furaha na huruma ya Mungu!


Wakleri na Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni mashuhuda amini wa Yesu Kristo, kwa njia ya furaha, upendo na huruma, changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika, Jumapili tarehe 8 Februari 2015 mjini Nazaret. Kardinali Baldisseri alitoa daraja la ushemasi kwa watawa wawili na daraja takatifu la Upadre kwa mtawa mmoja.

Katika mahubiri yake, Kardinali Baldisseri anasema, Mwenyezi Mungu anaendelea kufanya hija katika maisha na historia ya binadamu, kwa kubisha hodi kwenye milango ya mioyo ya waja wake, akiomba kuingia na kufanya makazi. Mwenyezi Mungu anabisha hodi katika uhuru wa mwanadamu, akiomba kukoleza mapendo yasiyokuwa na mipaka.

Katika mchakato huu, kuna waamini ambao wamethubutu kufungua malango ya maisha na mioyo yao, wakaonja huruma na upendo wa Mungu, leo hii ni wahudumu wa Injili ya Furaha. Lakini pia Mwenyezi Mungu amegonga kisiki kwa baadhi ya watu, kwani wameshindwa kumfungulia malango ya maisha yao na Mungu amebakia nje na matokeo yake, watu wamekosa kuonja furaha na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Baldisseri anawakumbusha Wakleri kwamba, maisha yao yanakuwa na thamani kubwa, pale wanapowashirikisha wengine furaha, matumaini na huruma ya Mungu; daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama alivyofanya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Mama Kanisa anawashukuru Watawa, Wazazi pamoja na Walezi wao, kwa kuwafunda vijana wao barabara, kiasi hata cha kuamua kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya maisha ya kitawa, kama: Mashemasi na Mapadre. Waamini wanaalikwa kuendelea kusali ili Bwana wa mavuno aweze kutuma watenda kazi wema na watakatifu katika shamba lake, viongozi watakaokuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo na Kanisa lake.

Inafurahisha kuona kwamba, hata leo hii kuna vijana wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Wakleri na Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia furaha na huruma ya Kristo kwa waja wake, kwani huu ndio wito na utume ambao wanapaswa kuutekeleza katika maisha yao kama Watawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.