Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kulinda na kutunza
mazingira ambayo kwa namna ya pekee kabisa yamepyaishwa na Kristo, kwa kumwondoa mwanadamu
kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; kwa kuwaponywa watu na magonjwa yao na hivyo
kuwapatia tena maisha mapya. Yesu katika maisha na utume wake alikuwa anakutana na
watu; wagonjwa walipomgusa mavazi yake wakaponywa na mateso pamoja na mahangaiko yao,
changamoto na mwaliko kwa waamini kudumu katika imani, kazi inayotekelezwa na Roho
Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha
Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 9 Februari 2015 anasema
kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kuumba, kazi inayobubujika kutoka katika upendo
wake na kwamba, mwanadamu anawajibika kulinda na kutunza mazingira, kwani amekabidhiwa
dhamana hii na wala si mmiliki wa kazi ya uumbaji.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanashiriki katika kulinda na kutunza
mazingira mintarafu sheria za nchi na wala si wajibu wa wakereketwa wa utunzaji wa
mazingira, ili kuendeleza kazi ya uumbaji pamoja na kujiachilia mikononi mwa Kristo
ili aweze kuwapatanisha, katika ngazi ya mtu binafsi, katika jumuiya pamoja na kuwapatanisha
na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, Roho
Mtakatifu anatenda kazi ndani mwao, ili kukua na kukomaa katika imani, matumaini na
mapendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.