2015-02-09 11:06:34

Utu wa mwanadamu!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu pendevu sana cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. RealAudioMP3

Tunakukaribisha tuendelee kuchota hekima kutoka katika hazina ya mafundisho ya mtaguso Mkuu wa II wa Vatican. Kukukumbusha tu ni kwamba, Mtaguso huu mkuu ulioitishwa na Mtakatifu Yohane wa XXIII, ulikuwa na lengo la kufungua madirisha ili kuleta hewa mpya ndani Kanisa, ili kuyapyaisha maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo maana tutakuta kwamba, wazee wa Mtaguso waligusa kila kona ya maisha ya Kanisa kwa undani wake.

Mpendwa msikilizaji baada ya kulimwilisha tamko lile liliyohusu uzito wa malezi katika kipindi kilichopita, leo tuitazame hati nyingine ambayo pia ni tamko kuhusu hadhi ya mwanadamu, kwa lugha ya Kilatini inakijulikana kwa jina la Dignitatis humanae. Maudhui msingi ya Dignitatis humanae ni juu ya Uhuru wa Dini. Kwa mantiki wazee wetu wa Mtaguso wanatazama Uhuru katika mambo ya dini kama ni sehemu ya kuheshimu hadhi ya Mwanadamu.

Msingi wa hadhi ya mwanadamu ni Mungu mwenyewe aliyependa kumwuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake. Hadhi na thamani ya Mwanadamu vipo katika asili yake babisa, siyo kitu anachopewa na mtu yeyote yule. Ni Mungu amependa kumshirikisha mwanadamu umungu wake na utakatifu wake. Na ndiyo maana mwanadamu safi, kwa msukumo wa kiu ya ndani ya roho, daima hujibidisha kutafuta Muungano na Muumba wake.

Ndani ya Dignitates humanae, wazee wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatazama kwa kina udhahiri wa mwanadamu na dini. Wakaaona kuwa dini sio kitu ambacho mtu hupewa, bali hutafuta kwa hekima ya moyo. Dini siyo kitu ambacho mtu hulazimishwa kufuata, bali kwa hiari ya moyo wake humtafuta na kumwelekea Muumba wake. Kwa mantiki hiyo, dini ni sehemu ya hadhi kabisa ya Mwanadamu na hivyo kila moja anapaswa kuheshimiwa katika hadhi yake hiyo. Wanakaza kusema, uhuru wa dini umejengwa katika maumbile ya mwanadamu mwenyewe. Siyo suala la kihisia au la kiitikadi. Ni kwa mantiki hiyo linapaswa kutazamwa kwa uzito wa pekee.

Kwa mawazo, mchanganuo, Dignitatis humanae inakazia juu ya haki ya mtu binafsi na ya jumuiya pia ya kuwa na uhuru wa kijamii na wa kiserikali katika masuala ya dini. Historia na nyakati zetu zinashuhudia jinsi ambavyo watu wananyanyaswa hata kudhulumiwa uhai wao kwa kulazimishwa kufuata itikadi fulani za kidini. Jambo hilo liwe linafanywa hadharani au kwa siri, au kwa propaganda ya aina yoyote ile linadhalilisha Hadhi ya mwanadamu.
Lakini katika tamko hili, Dignitatis humane, Hadhi ya mwanadamu, Wazee wa Mtaguso wanaangazia pia suala la uhuru wajibifu. Kwa sababu sisi binadamu ni viumbe jamii basi, uhuru wetu katika kufikiri, kupanga na kuamua lazima uheshimu mipaka, uheshimu utu na uwepo wa wengine pia. Migogoro na migongano inakuja pale ambapo baadhi wanatumia vibaya uhuru wao, huku wakikanyagakanyaga uhuru wa wengine. Kimsingi, hakuna mtu mwenye uhuru wa kufanya kila kitu anachowaza na kutaka. Uhuru wetu uratibishwe na heshima yetu kwa Mungu na kwa wanadamu wenzetu. Uhuru wetu utusaidie kutenda mambo kwa manufaa ya wote.

Ikikazia mafaa ya wote Dignitatis humanae, hadhi ya mwanadamu inakaza kusema, watu lazima waheshimu kanuni za kimaadili na uwajibikaji wa mtu binafsi na wa kijamii. Katika kuzitumia haki binafsi ni lazima pia kujali haki za wengine. Na hayo yote yaongozwe kwa dhamiri safi, hai na wajibifu mbele za Mungu na wanadamu. Hadhi ya Mwanadamu, Uhuru na uwajibikaji makini wake ndiyo mambo msingi yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana usitawi wa jumuiya ya watu, kiroho na kimwili.

Mpendwa msikilizaji, Dignitatis humanae inakufuata hapohapo unapoishi na kufanya kazi. Inakukumbusha kuwa wewe ni kiumbe huru wa Mungu, ishi kwa uhuru unaokusaidia kujenga na kulinda thamani yako kama mwanadamu. Uhuru huo utusaidie kumtafuta Mungu, kumpenda na kumtumikia kwa umakini zaidi katika nyanja mbalimbali za maisha yetu, tukianzia katika familia zetu na maisha ya kawaida ya mahusiano jamii. Fundisho msingi hapa ni hili, kabla hujamtendea lolote mwenzako, kwanza kabisa kumbua kuwa huyo ni binadamu.

Hadhi ya ubinadamu wake itangulizwe mbele kabisa ili usije ukakosea, ukaunyanyasa utu wake kwa kigezo cha upendo. Endapo wewe unataka mie nikusikilize na kutii tu vile unavosema na kutaka, hapo unanishusha hadhi. Mimi ni mtu, na wewe mtu mwenzangu uwe tayari kunisikiliza. Endapo wewe unataka mimi nikuheshimu tu, na wewe hutaki kuniheshimu, hapo ndugu yangu unanipunguza thamani. Endapo wewe unajiona ni mwenye haki zaidi kuliko mimi, na haki zako unazitetea hata kwa njia ya kukanyaga pua za sie wenzio, hapo unatupunguza thamani.

Hii ni moja ya kanuni inayosaidia kulinda hadhi ya mwanadamu, iwe ni katika familia au popote pale tuishipo watu. Tuonane, tutambuane, tuthaminiane, tusaidiane, tuelekezane kwa upendo, tuvumiliane, tuinuane, tushikane mikono – twende pamoja. Ni hapo tu sote tutakuwa na furaha. Tusipunguzane thamani bwana! Thamani na hadhi yangu sio mali yako ni ya Mungu. Unisaidie kuitunza hadhi yangu na mimi nitakutendea vivyo hivyo kwa ajili ya heshima ya Mungu!

Yote hayo yajengwe katika uhuru wetu katika Bwana, uhuru wa watoto wa Mungu. Kwa bahati mbaya kubwa sana, leo hii watu wengi wanafikiri kuwa huru ni kumkimbia Mwenyezi Mungu, kuenenda katika njia zao peke yao huku wakiongozwa na dhamiri butu na akili tundu zinazowapelekea katika harufu ya kifo cha mwili na roho. Ndiyo maana tunajitendea na kutendeana matendo ya ajabu na wakati mwingine tunashetanishana kabisa, huku tunasahau thamani na maana ya maisha yetu, tunapuuza thamani ya mwanadamu, mwanadamu anageuzwa kuwa kitu tu cha kuburuzwa, kupuuzwa na kutendewa kikatiri kama tunavyoshuhudia katika ulimwengu wetu leo.

Na kwa kujiweka mbali na Mungu, tunaukosa ufunuo wa Kimungu wa kutusaidia kujua Mungu anataka nini kwetu. Badala yake wapo wengi leo hii ambao wamegeuza dini kuwa ni kitega uchumi chao. Wataanzisha makundi ya ibada, ili kukusanya pesa. Ikitokea hivyo, hadhi ya mwanadamu na heshima ya Mungu, vyote huangamizwa. Dini siyo biashara, kubiasharisha dini ni kudhihaki heshima ya Mungu!

Kwa mwangwi wa Dignitatis humanae, tukazie maarifa kusema kuanzi katika malezi ya mwanzo kabisa mwanadamu afundishwe namna ya kutenda kwa kujiheshimu mwenyewe na kuwaheshimu wenzake. Uhuru katika kutenda, uchochee zaidi thamani ya Mwanadamu. Cheche za tamko hili, Dignitatis humanae, zitusaidie sana kukwepa kishawishi cha watu wa nyakati zetu, ambao kwao uhuru wa mwanadamu ndiyo kigezo cha kuwa watenda maovu hodari. Zipo hata taasisi zisizojali utu, ambao kwao matendo yao maovu na mifumo dhambi wanaoiweka, wanaipa sura ya ‘haki ya binadamu’. Wanaunda na kuhalalisha mifumo-angamizi kwa kudai kuwa hizo ni haki za binadamu. Kwa nini hivi? Kwa sababu tunatumia vibaya uhuru wetu wa akili mwili na roho hadi tunasahau utu wetu.

Dignitatis humane inatualika wewe na mimi, kusimama kidete kueleza, na kulinda thamani ya mwanadamu, na kuhimiza matumizi ya uhuru wetu kwa manufaa ya wote, ni kwa namna hiyo tutachangia zaidi katika kuienzi thamani ya mwanadamu.

Kutoka katika studio za Radio vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.