2015-02-09 09:20:05

Papa Francisko kuhutubia Congress ya Marekani, 24 Septemba!


Familia ya Mungu Jimbo kuu la Washington, nchini Marekani limepokea kwa furaha na bashasha kubwa taarifa inayosema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Marekani, mwezi Septemba, 2015, tarehe 24 Septemba, atahutubia Baraza la Congresi la Marekani. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhutubia wajumbe wa Congresi.
Taarifa hii imetolewa na Mheshimiwa John Boehner. Tukio hili la kihistoria utakuwa ni wakati wa furaha na neema na kwamba, Familia ya Mungu nchini Marekani kwa sasa inasubiri kwa hamu na matumaini makubwa mpango mzima wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Marekani, ili waweze kujipanga kikamilifu kumpokea na kumkarimu mgeni huyu maalum anayeendea kukonga nyoyo za watu wengi kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake.
Itakumbukwa kwamba, Jimbo kuu la Washington lina Wakatoliki zaidi ya 620, 000 wanaoishi katika Parokia 139. Jimbo linamiliki na kuendesha shule 95 ndani ya Jiji la Washingtown DC na kwenye vitongoji vyake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.