2015-02-09 09:24:37

Mpeni nafasi Yesu, ili awainjilishe!


Maisha ya Yesu Kristo yalijikita katika kuwafundisha watu Habari Njema ya Wokovu, kuponya wagonjwa na kuwaondolea watu dhambi zao. Katika Ibada ya Misa Takatifu, waamini wanajiweka mbele ya Yesu, kiongozi mkuu wa Ibada inayoadhimishwa na Wakleri, kwani Yesu Kristo ndiye Kuhani mkuu anayejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti, changamoto kwa waamini kujiweka mbele ya Yesu na kumsikiliza kwa makini, ili aweze kuwamegea Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Parokia ya San Michele Arcangelo Pietralata, iliyoko Jimbo kuu la Roma, Jumapili jioni tarehe 8 Februari 2015, amewataka waamini kujibidisha kutafuta, kusikiliza, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku, hata kama ni kwa dakika chache, kwani Yesu ni Neno la uzima. Waamini wajifunze kusali kwa kutumia Neno la Mungu, kwani Yesu anataka kuwaponya waja wake kutokana na madonda ya mwili na roho katika maisha yao pamoja na kuwaondolea dhambi zao. Waamini wajitahidi kumfungulia Yesu Kristo mioyo yao, kwa njia ya sala, ili aweze kweli kuwaponya.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na watoto pamoja na vijana wa katekesi Parokiani hapo amewaambia kwamba, Shetani ni kiini cha vita, chuki na kinzani katika jamii, lakini Mwenyezi Mungu ni kiini cha: amani, mapendo, umoja na mshikamano wa kweli. Vita vinavyoendelea sehemu mbali mbali za dunia ni matokeo ya chuki kati ya watu, Yesu anapenda kupandikiza mbegu ya haki na amani kati ya watu. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wajitahidi kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuongoza maisha yao.

Baba Mtakatifu anawataka watoto na vijana hawa wa katekesi kujifunza kusali vyema zaidi na kwamba, wito na maisha ni mambo yanayohitaji sadaka, ari na moyo wa kujinyima kwa ajili ya kupata usalama na utulivu wa ndani. Mwanadamu ataendelea kukabiliana na matatizo, changamoto, lakini pia fursa za kuweza kupata furaha na utulivu katika maisha na wito wake, jambo la msingi ni kujenga na kukuza uvumilivu, imani na matumaini.

Baba Mtakatifu pia alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wazazi, walezi na watoto ambao wamebatizwa siku za hivi karibuni, kwa kuwataka wazazi kuwa ni watangazaji wa Injili ya Uhai, kwa kuhubiri kuhusu maisha na kwamba, wanao wajibu wa kuwalea watoto wao katika imani, maadili na utu wema. Wazazi wajitahidi kuwalea na kuwapatia watoto wao katekesi makini katika hija ya maisha yao ya kila siku, lakini zaidi kwa njia ya mifano bora ya maisha.

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea kwenye Ibada ya Misa, alisimama na kusalimiana na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanaohudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Amewashukuru kwa ukarimu na mapokezi mazuri waliyomwonesha na kuwataka kuendelea kubeba Msalaba wa maisha kwa imani na matumaini, kwani Roho Mtakatifu yuko daima pamoja nao!

Baba Mtakatifu pia amekutana na kuzungumza na wagonjwa, na kuwataka daima kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu hata katika shida na mahangaiko yao ya ndani; daima anawapenda na kuwalinda. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaomba waamini kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.