Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto iliyokutana kwa mara ya kwanza tangu
kuundwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 Februari,
2015, imemaliza mkutano wake kwa wajumbe kushirikishana uzoefu, ujuzi na mang'amuzi,
ili kuweza kumsaidia Baba Mtakatifu katika kubainisha mikakati na kanuni za kuwalinda
watoto wadogo ndani ya Kanisa.
Wajumbe kutoka katika makundi mbali mbali wameshirikisha
taarifa ya taaluma waliyoifanyia kazi kwa miaka kadhaa iliyopita. Wajumbe wamekamilisha
muundo wa tume na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili
ya uamuzi na utekelezaji zaidi. Wajumbe wataendelea kufanya tafiti na miradi mbali
mbali mintarafu utume na dhamana waliyokabidhiwa na Kanisa, ili kweli watoto waweze
kupata mazingira bora na salama.
Mkakati huu unapania pamoja na mambo mengine
kutoa huduma za kichungaji kwa wahanga wa nyanyaso za kijinsia pamoja na familia zao;
elimu, miongozo, majiundo makini kwa Wakleri na Watawa; sheria za Kanisa na kiraia
kuhusu nyanyaso za kijinsia pamoja na wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kukabiliana
na tuhuma za nyanyaso za kijinsia. Uwajibikaji wa viongozi wa Kanisa ni muhimu sana,
lakini wajibu huu unapaswa pia kutekelezwa Wakleri, Watawa na Walei wanaowahudumia
watoto kadiri ya shughuli zao.
Kwa kuzingatia unyeti wa tatizo lenyewe, kuna
haja kwa Kanisa katika ngazi mbali mbali kuwa na uelewa mpana zaidi, jambo ambalo
linahitaji semina kama sehemu ya mchakato unaopania kuwajengea viongozi wa Kanisa
kanuni na uelewa zaidi ili kuwalinda watoto wadogo. Tume inaandaa pia siku maalum
ya kusali kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa nyanyaso za kijinsia, ili watu watambue
kwamba, kweli Kanisa linapania kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.