2015-02-09 08:29:24

Mheshimiwa Padre Amisse Canira ateuliwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Lichinga, Msumbiji


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Elio Greselin, S.C.I wa Jimbo Katoliki Lichinga, Msumbiji la kung'atuka kutoka madarakani kadiri ya Sheria za Kanisa namba 401ยง Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Amisse Canira kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Lichinga.

Askofu mteule Amisse Canira alizaliwa kunako tarehe 2 Mei 1962 Jimboni Nacala, mara baada ya masomo, malezi na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 12 Desemba 1993, akiwa ni Padre wa kwanza mzalendo kutoka katika eneo hili.

Baadaye katika maisha na utume wake kama Padre amekuwa ni Paroko kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1996. Baadaye alitumwa mjini Roma kwa masomo ya juu kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 1998 na kujipatia Shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha maadili cha Alfonsiana. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001 alikuwa ni Paroko wa Kanisa kuu la Nacala.

Mwaka 2002 hadi mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Baba wa maisha ya kiroho Seminari kuu ya Mtakatifu Pio X, Maputo. Kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2010 alikuwa Paroko, Makamu Askofu na mkurugenzi wa Utume wa Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji kwa kipindi cha miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2004.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.