Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto imehitimisha mkutano wake wa kwanza
uliokuwa unafanyika mjini Vatican chini ya uongozi wa Kardinali Sèan Patrick O’Malley,
Rais wa tume hii aliyewataka viongozi mbali mbali wa Kanisa kushirikiana na tume,
ili kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia, kwa
kufungua ukurasa mpya wa upatanisho na uponyaji kwa wale wote walioguswa na mkasa
huu.
Ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kama anavyosisitizia Baba Mtakatifu
kuhakikisha kwamba, wanaunda mazingira yatakayowahakikishia watoto usalama wa maisha
yao sanjari na viongozi hawa kukutana, kuzungumza, kuwasaidia pamoja na kuomba msamaha.
Mambo ambayo yamepewa mkazo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake
kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ulimwenguni na kwa wakuu wa Mashirika ya Kitawa
na Kazi za Kitume. Ni wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu kuunda tume itakayobainisha dira
na mwongozo wa kupambana na nyanyaso za kijinsia.
Tume hii itakuwa inashirikiana
na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, itakayotoa mwongozo na suluhu makini
ya kukabiliana na matatizo kama haya yanapojitokeza. Ni jukumu la Tume hii kuandaa
sera na mikakati ya elimu na majiundo makini itakayokuwa na programu na mbinu za kuwalinda
watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.
Kardinali Sèan Patrick O’Malley
anasema, kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa
watoto, wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia walioteuliwa na Baba Mtakatifu
Francisko wameshiriki kwa ukamilifu kwa kuchangia mawazo, uzoefu na mang’amuzi yao
katika mchakato wa mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo.
Tume
kwa sasa inaandaa semina ili kuwajengea uwezo viongozi wa Kanisa katika mikakati ya
kuwalinda watoto; semina zitakazotolewa kwa viongozi wa Sekretarieti ya Vatican pamoja
na Maaskofu wapya wanaofika mjini Vatican kila mwaka kwa ajili ya kupata semina elekezi
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu
wa Mungu majimboni mwao.
Tume inaendelea kuandaa vitini kwa ajili ya sala
kwa watu walioguswa na mkasa huu katika maisha yao kama sehemu ya mchakato wa uponyaji
wa maisha ya kiroho pamoja na kuhamasisha waamini kutambua madhara na athari za nyanyaso
za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.
Tume pia inaanza kutafuta fedha kutoka
kwa Mashirika mbali mbali ya misaada ili kuwasaidia waathirika wa nyanyaso za kijinsia
pamoja na mafunzo. Tume inapania kushirikiana na waathirika wa nyanyaso za kijinsia
ili kusaidia kutoa mawazo ya kuwakinga watoto pamoja na miongozo makini.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.