2015-02-09 08:50:29

Kusoma, Kuandika na Kuhesabu vyawekewa mkakati maalum!


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amezindua Mpango wa Kitaifa wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unaolenga kukuza viwango vya uelewa kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili nchini Tanzania. Mpango huo wa miaka mitatu ulioanza kutekelezwa 2014/2015 hadi 2016/2017 umelengwa kuwahusisha watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13 walio kwenye mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi (MEMKWA).

Akizungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi walioshiriki uzinduzi huo Jumamosi, Februari 7, 2015, Waziri Mkuu Pinda alisema mpango huo ni mkubwa na umeandaliwa mahsusi kujibu changamoto zilizojitokeza miaka ya nyuma. Aliwataka watekelezaji wakuu wa mpango ambao ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuhakikisha kuwa wanazishirikisha asasi zisizo za Kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya elimu.

“Kuna mashirika mengi yasiyo za kiserikali ambayo ni chachu ya kuhimiza elimu nchini... jaribuni kuwashirikisha sababu wao ni wadau wazuri sana wa suala hili. Pangeni utaratibu wa kukaa na hawa wadau na kuwapa mrejesho wa mpango huu mzima,”alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wahusika wakuu wa mpango waangalie mgawanyo wa mikoa iliyoingizwa kwenye mpango huo kwa kuzingatia kanda ili kuleta matokeo ya mtawanyiko badala ya hali ilivyo sasa. “Nimeangalia jinsi mlivyogawa mikoa yenu, inanipa taabu kidogo... kuna mikoa inahitaji msukumo wa pekee, mikoa ya wadugaji, mikoa iliyoko pwani ya bahari na maziwa, yote inahitaji msukumo wa tofauti,” alisema.

Katika taarifa yao, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisema mpango huo wa KKK au LANES (Literacy and Numeracy Support Programme) unafadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu (Global Partnership for Education – GPE) na wahisani wengine.
Wahisani hao ni pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) kupitia mradi wa EQUIP-T unaotekelezwa katika mikoa saba ya Kigoma, Shinyanga, Mara, Simiyu, Lindi, Dodoma na Tabora; Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu kwa Mtoto (UNICEF) wanaofadhili utelekezaji wa Mpango wa LANES katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe; na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia Mradi wa TZ-21 unaotekelezwa katika mkoa wa Mtwara.
Mapema, akisoma taarifa ya mpango huo mbele ya Waziri Mkuu, Kamishna wa Elimu nchini, Prof. Eustella Bhalalusesa alisema mpango huo umelenga kuongeza ufanisi katika stadi za KKK, kurahisisha kazi ya walimu wanaofundisha watoto wa darasa la kwanza na la pili pamoja na kuongeza ushiriki wa jamii katika kuboresha elimu na hasa ujifunzaji wa stadi za KKK.
Alisema mpango huo utachangiwa sh. bilioni 150 ambazo zitaingizwa moja kwa moja kwenye mfuko wa elimu kupitia Wizara ya Fedha.
Alisema maandalizi yote ya utekelezaji wa mpango huu yamekamilika ikiwa ni pamoja na mtaala wa darasa la kwanza na darasa la pili, muhtasari wa KKK kwa darasa la I & II, pamoja na Mwongozo wa Mwalimu wa kufundisha kusoma kuandika na kuhesabu.








All the contents on this site are copyrighted ©.