2015-02-09 10:11:05

Dumisheni haki na usawa!


Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupambana kikamilifu na baa la njaa na umaskini wa hali na kipato; mambo ambayo yanaendelea kunyanyasa watu wengi duniani, kuna haja ya kujifunga kibwebwe ili kungo’a mambo yale yanayosababisha ukosefu wa usawa wa kijamii.

Kuna watu ambao wanaendelea kuteseka kutokana na baa la njaa duniani, lakini wakati huo huo kuna watu wanakula na kusaza, hapa shida ni ukosefu wa mfumo bora wa ugawaji na usambazaji wa chakula duniani, hali ambayo inapelekea uharibifu mkubwa wa chakula. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuliangalia tatizo hizi na kulifanyia kazi, ili kweli baa la njaa liweze kushughulikiwa kikamilifu, kwa njia ya haki na mshikamano.

Ni changamoto ambayo imetolewa Jumamosi, tarehe 7 Februari 2015 na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Serikali ya Italia kama sehemu ya maandalizi ya Onesho la Chakula Duniani kwa mwaka 2015 linalojulikana kama Expo 2015. Kongamano hili ambalo limefanyika mjini Milano, Kaskazini mwa Italia limengozwa na kauli mbiu “Expo ya mawazo mfumo wa kiitalia katika kulisha dunia kati ya mbinu mpya na endelevu”.

Baba Mtakatifu anasema, ili Jumuiya ya Kimataifa kuweza kukabiliana na changamoto za baa la njaa na umaskini duniani, kuna haja ya kujikita katika mambo makuu matatu: kipaumbele cha kwanza dhidi ya umaskini; ushuhuda wa upendo na utunzaji bora wa mazingira.

Kwanza kabisa, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inajiwekea mikakati endelevu na inayotekelezeka katika kupambana na baa la umaskini duniani, kwa kung’oa mambo yote yanayosababisha watu kuendelea kuogelea katika baa la umaskini na njaa duniani; hapa jambo la kwanza ni kujenga misingi ya haki na usawa kati ya watu. Ili kufanikisha mkakati huu, kuna haja ya kubomoa haki miliki ya masoko, tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutaka kujipatia faida kubwa katika mfumo wa fedha na uchumi sanjari na kurekebisha miundo mbinu inayokwamisha harakati za ujenzi wa usawa katika Jumuiya ya Kimataifa.

Pili, anasema Baba Mtakatifu ni kuendelea kurekebisha mfumo wa sera na mikakati ya kiuchumi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima ya binadamu na mafao ya wengi. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuwa ni dira na mwelekeo wa uchumi bora duniani, lakini kwa bahati mbaya ni mambo ambayo kamwe hayapewi uzito wa kutosha katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Baba Mtakatifu anawataka wachumi na watunga sera kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya mwanadamu sanjari na kujielekeza kwa ajili ya utekelezaji wa mafao ya wengi.

Tatu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho badala ya mtindo wa sasa wa maisha unaochangia uharibifu mkubwa wa mazingira, kiasi cha kutishia maisha ya watu wengi duniani. Matumizi bora ya ardhi yamsaidie mwanadamu kupata mahitaji yake msingi pamoja na kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira. Hii ni dhamana ya kila mtu duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.