Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, hivi karibuni akiwa
mjini Nazareth amewashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa kutoka Nchi Takatifu pamoja
na familia kuhusu maendeleo ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu
familia inayotarajiwa kufanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2015. Familia zinazoishi
katika Nchi Takatifu zinahitaji kujikita katika fadhila ya matumaini kwani zinakabiliwa
na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali kama zilivyofafanuliwa na viongozi wa
Kanisa wakati wanashirikisha mawazo, tafakari na maoni katika kongamano hili lililoandaliwa
kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia
iliyofanyikwa mjini Vatican kunako mwaka 2014. Matatizo na changamoto za kisiasa
na kiuchumi; ukosefu wa amani, usalama na utulivu; ukosefu wa fursa za ajira; changamoto
za malezi kwa watoto wanaozaliwa katika ndoa mseto; tatizo la wahamiaji; changamoto
na athari za mitandao ya kijamii katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Kuna changamoto za majadiliano ya kiekumene katika masuala ya kifamilia kwa waamini
wanaohamia kwenye Makanisa mengine ya Kikristo; tatizo la kushiriki kikamilifu katika
maisha ya Kisakramenti: hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na ile ya Upatanisho.
Bado kuna ukiritimba wa kupata haki kwa wanandoa ambao wanakabiliwa na mashaka ya
uhalali wa ndoa zao. Kardinali Baldisseri anabainisha kwamba, hati ya Mababa wa
Sinodi ya Maaskofu iliyohitimishwa mwaka 2014 inapembua kwa kina na mapana mada mbali
mbali zilizowasilishwa katika kongamano hili mintarafu hali halisi ya maisha ya ndoa
na familia huko Mashariki ya Kati. Hati hii imekuwa ni sehemu ya mwongozo uliotumwa
kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, ili uweze kujadiliwa, tayari kuanza mchakato wa
Hati ya Kutendea Kazi, yaani, “Instrumentum Laboris”. Mang’amuzi ya maadhimisho
ya Sinodi maalum kwa ajili ya familia, lilikuwa ni tukio la neema na baraka kwa maisha
na utume wa Kanisa, kama alivyofafanua Baba Mtakatifu Francisko. Mababa wa Sinodi
walitambua na kuguswa na matumaini, matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazozikabili
familia. Mababa wa Sinodi walimshukuru Mungu kwa uaminifu unaotekelezwa na familia
nyingi katika maisha na utume wao kama familia za Kikristo, licha ya matatizo, changamoto
na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza mbele yao. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.