Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaonesha wasi wasi wake kutokana na kuongezeka
kwa gharama ya elimu nchini humo, hali ambayo inatishia mchakato wa wananchi wengi
kupata elimu bora kwa kiwango cha gharama wanachoweza kumudu, hata maskini na watu
wenye kipato cha kawaida.
Ongezeko la ada kwa shule za Serikali kuna hatarisha
kukwamisha juhudi za kuwapatia elimu watoto wote wa Kenya na kwamba, ni wajibu na
jukumu la Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, watoto wote wanapata elimu. Si haki
watoto wa maskini kunyimwa haki ya kujipatia elimu kwa kukosa ada ya kulipia gharama
za elimu nchini Kenya, wanasema Maaskofu.
Serikali iangalie namna ya kuwasaidia
watoto wa maskini hata wao kupata elimu, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ili
kuangalia uwezekano wa kugharimia elimu kadiri ya gharama ya maisha ya wananchi wengi
wa Kenya. Elimu ni wajibu wa wananchi wote wa Kenya, jambo ambalo pia linahitaji sheria
makini, uwajibikaji, ukweli na uwazi, kwani ongezeko la gharama za elimu kutakwamisha
utoaji wa elimu, kwani gharama ya maisha kwa sasa iko juu sana, wakati hali ya maisha
ya wananchi wengi wa Kenya inaendelea kudidimia anasema Askofu Maurice Crwowley, Makamu
mwenyekiti, Tume ya elimu na elimu ya dini, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.