2015-02-07 15:01:17

Wainjilisheni watu wa mijini!


Baraza la Kipapa kwa ajli ya Walei kwa kipindi cha mwaka mzima, limekuwa likijitahidi kutekeleza mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwa kutumia Waraka wa Injili ya Furaha, Evangelii gaudium, kuwa ni dira na mwongozo wake sanjari na mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50, tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu: Utume wa Walei ndani ya Kanisa, "Apostolicam actuositatem" changamoto endelevu hata kwa siku za usoni.

Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Walei, Jumamosi, tarehe 7 Februari 2015, baada ya kuhitimisha mkutano wao wa mwaka, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Kukutana na Mwenyezi Mungu katikati ya Jiji", kama changamoto ya utekelezaji wa Waraka wa Injili ya Furaha inayolitaka Kanisa kukabiliana kikamilifu na changamoto za utamaduni wa mijini; hali ambayo inaendelea kupanuka na kushika kasi kama sehemu ya utandawazi, kwani watu wengi kwa sasa wanaishi mijini.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, maisha ya mijini yanaathari kubwa katika akili, tamaduni, mifumo ya maisha, mahusiano kati ya watu na maisha ya kiroho. Kumbe, hapa Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji, ili kukabiliana na matatizo na changamoto zinazojitokeza, kiasi hata cha kuhatarisha utu, heshima na furaha ya binadamu; mambo yanayochangia ongezeko la umaskini, ukosefu wa makazi bora pamoja na mahusiano tenge ya kijamii, kiasi kwamba, kuna baadhi ya watu wanaishi katika mazingira duni katika miji na majiji.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, hata katika mazingira kama haya, mwanadamu anapaswa kukumbuka kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuonesha utashi wa kukutana na mwanadamu hata katikati ya miji, jambo la msingi ni waamini kutomgeuzia Mungu kisogo katika maisha na mipango yao, kwani Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao, ili kuwaonesha maana ya maisha, huduma inayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini walei, kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha, katika medani mbali mbali za maisha, dhamana inayotekelezwa na mtu mmoja mmoja, familia, jumuiya au chama cha kitume. Waoneshe ujasiri wa kutaka kukutana na watu, ili kuleta mabadiliko katika maisha yao. Watambue kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mdau mkuu wa Uinjilishaji na anaendelea kuandaa mioyo ya watu ili kupokea Injili ya Furaha.

Hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini walei wanapata majiundo makini katika misingi ya imani, matumaini na mapendo, kwa kuhamasishwa kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha yao, tayari kumshuhudia Kristo kama kielelezo cha imani tendaji. Mama Kanisa kwa njia ya unyenyekevu anataka kuyachachusha malimwengu kwa njia ya maisha ya Wakristo wanaoishi mijini.

Waamini walei waendelee kushirikiana na kushikamana na viongozi wao wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wao ni muhimu katika utekelezaji wa dhamana hii, kama alivyokuwa anakazia Mwenyeheri Paulo VI, wakati huo akiwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano. Watu watangaziwe Habari Njema ya Wokovu, inayojikita katika upendo wa Mungu na Wokovu unaoletwa na Yesu Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.