2015-02-07 14:59:13

Kanisa Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Piliwa Vatican kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, kwa kuwa na sauti moja sanjari na kuendelea kuwa chombo cha wokovu, amani, majadiliano na upatanisho.

Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu, SECAM haina budi kuwa aminifu kwa utambulisho wake kama kielelezo hai cha umoja na huduma hasa miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa viongozi wa Kanisa hawana budi kuwa makini katika maisha na utume wao, na kamwe wasimezwe na malimwengu, bali kwa kuendelea kushirikiana na kwa karibu zaidi na Balozi za Vatican zilizoko Barani Afrika pamoja na kudumisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kushirikishana uzoefu na mang'amuzi ya kikanisa na shughuli za kichungaji, daima Kanisa likijitahidi kuwa karibu na watu!

Ni changamoto na wosia unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Viongozi wakuu wa SECAM, alipokutana na kuzungumza nao, Jumamosi, tarehe 7 Februari 2015 mjini Vatican, baada ya kuhitimisha mkutano wa SECAM uliokuwa unafanyika mjini Vatican. Vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu wanahitaji ushuhuda, changamoto ya kutoshikamana sana na mambo ya utajiri, mali, madaraka, mafanikio na misimamo mikali ya kidini.

Ili kuwasaidia vijana Barani Afrika kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kuna haja ya kuwekeza katika sekta ya elimu, ili kuwajengea watu nidhamu, haki, amani na utulivu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha na utu wema. Mchakato wa maboresho katika sekta ya elimu, hauna budi kwenda sanjari na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa vijana, ili waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kuna mambo mengi yanayochangia kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, lakini inapaswa kukumbukwa kwamba, Familia ni chemchemi ya udugu na msingi wa amani; changamoto kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwekeza katika Injili ya Uhai, kwa kuwasaidia wagonjwa, walemavu, wazee pamoja na kuzijengea uwezo familia ili ziweze kukabiliana na dhamana yake barabara.

Kanisa Barani Afrika limeendelea kuwa kweli ni shuhuda wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa Wakristo kujisadaka kwa ajili ya jirani zao katika medani mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu anaipongeza na kuishukuru Familia ya Mungu Barani Afrika kwa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu wakati wa kukabiliana na janga la Ebola, ambalo limekuwa kweli ni tishio kwa maisha na maendeleo ya watu wengi Barani Afrika. Kanisa liendelee kuwekeza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kuamsha dhamiri za viongozi wa kisiasa na kijamii, ili waweze nao kuchangia katika maboresho ya maisha ya watu wao.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wamissionari wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume yanayotekeleza utume wake Barani Afrika. SECAM ni chombo cha sheria, ili kusaidia kuponya madonda ya rushwa na ufisadi, ili kukoleza mchakato wa kutafuta na kukumbatia mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, Uinjilishaji ni dhamana na wajibu wa kila Mkristo, ili iweze kuenea na kuwafikia watu wengi zaidi. Uinjilishaji unajikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuiamini Injili; dhamana inayopaswa kutekelezwa na Jumuiya nzima ya waamini, ili kuimarisha imani na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.