2015-02-07 08:46:31

Elimu kwanza!


Kuna haja ya kuthamini tofauti zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa dhati na kwamba, hakuna mabadiliko ya kweli yanayoweza kufanywa katika maisha ya binadamu bila kuzingatia elimu! Mabadiliko katika mfumo wa elimu ni kikolezo kikuu cha maendeleo ya mwanadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya familia, shule, jamii na tamaduni za watu, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa katika maisha ya mwanadamu. Wadau mbali mbali katika sekta ya elimu wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, wamekabidhiwa amana na utajiri mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya sasa na kwa siku za usoni.

Mafanikio, matatizo na changamoto zipembuliwe kwa uadilifu mkubwa, ili kupata matokeo yanayokusudiwa katika mchakato wa kuleta maboresho katika mfumo wa elimu, ili kweli mwanadamu aweze kufikiri vyema na kutenda kile anachofikiri kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa maboresho ya elimu, ili kweli elimu iweze kuwa na manufaa kwa vijana wa kizazi kipya, tayari kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa haki, amani na mshikamano.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo na wanafunzi wenye ulemavu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama tukio la kufunga mkutano mkuu wa nne wa mitandao ya shule za kimataifa, unaojulikana kama "Scholas Occurrentes" ulioanzishwa na Kardinali Jorge Mario Bergoglio, wakati huo akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina, leo hii mtandao huu unajumla ya shule 4000, zilizoenea sehemu mbali mbali za dunia. Mtandao huu unawajumuisha wanafunzi katika masuala ya michezo, sayansi na teknolojia. Mkutano huu ulikuwa unafanyika mjini Roma.

Baba Mtakatifu anasema, kila mwanafunzi ni hazina muhimu sana inayopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa. Vijana hao kwa njia ya video wamesilimua shida, matatizo na changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku. Lakini bado wameweza kuvuka magumu yote haya kwa njia ya matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii pasi na kukata tamaa.

Mchakato wa mageuzi ya elimu unaweza kusonga mbele kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika kukuza na kudumisha mila na tamaduni njema za kijamii; kwa kuendeleza michezo, ili kuibua karama na vipaji mbali mbali miongoni mwa vijana, tayari kusaidia maboresho ya maisha ya vijana bila kusahau umuhimu wa kuwajengea vijana maarifa na ujuzi katika masuala ya sayansi; mambo ambayo yanaweza kuwa ni madaraja ya kuwaunganisha watu katika jamii.

Vijana wajifunze kuheshimu na kuthamini mila na tamaduni zao njema, wasiwe ni watu wa kuiga na kuchukua kila jambo kwani wanaweza kugenishwa hata katika tamaduni zao wenyewe! Vijana pia wajitahidi kutafuta hekima ya Kimungu inayojikita katika Maandiko Matakatifu; katika sanaa na uzuri, ili kukoleza kipaji cha ugunduzi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawaalika wanafunzi kuonesha utajiri unaofumbatwa katika maisha yao, ili kuwashirikisha na kuwamegea wengine, ili hazina hii iweze kuzaa matunda na kuongezeka zaidi.Wajitahidi kujenga na kudumisha amani na utulivu ndani mwao, kwa kuonesha uvumilivu, kwa kukubali mapungufu sanjari na kuheshimu tofauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.