Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, Jumapili tarehe 8 Februari, 2015 linaadhimisha
Siku ya Mshikamano Kitaifa, ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Shirika la Misaada
la Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, "Manos Unidas" katika mapambano dhidi ya
baa la umaskini duniani, janga ambalo linaendelea kunyanyasa na kudhalilisha mamillioni
ya watu sehemu mbali mbali za dunia.
Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli
mbiu" Mapambano dhidi ya baa la umaskini". Maaskofu wanawahamasisha waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kujinyima kidogo, kwa ajili ya kusaidia kasi ya mchakato wa
mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani, sanjari na ongezeko la njaa na utapiamlo,
kashfa ya karne ya ishirini na moja!
Maaskofu wanasema, kuna kundi kubwa la
watoto wanaoteseka na kufariki dunia wakiwa na umri mdogo kutokana na utapiamlo wa
kutisha. Hili ni jambo la kusikitisha kwani kuna sehemu za dunia watu wanakula na
kusaza, kiasi hata cha kujaza mapipa ya taka kwa chakula ambacho, kingeweza kusaidia
mapambano dhidi ya utapiamlo wa kutisha, hapa kinachojitokeza ni utamaduni wa utandawazi
usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyobainisha Baba Mtakatifu
Francisko.
Watu wakijiondoa katika ubinafsi, wakaanza ujenzi wa mshikamano
wa udugu na upendo, kwa kuongozwa na dhamiri safi na nyofu; umaskini na njaa ni mambo
yanayoweza kupewa kisogo na Jumuiya ya Kimataifa. Hapa kuna haja ya kubadili sera
na mifumo ya kisiasa na kiuchumi, ili kupambana kufa na kupona na baa la njaa na umaskini
wa hali na kipato! Umaskini si jambo la kudekezwa, kwani madhara yake ni makubwa katika
maisha na maendeleo ya watu!
Maaskofu wanasema kwamba, ujenzi wa mshikamano
wa upendo ni agizo la Kiinjili ambalo linapaswa kuvaliwa njuga na Familia ya Mungu,
kwani watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zao katika shida na mahangaiko yao
ya ndani. Kumbe, hapa kuna umuhimu wa kuelimisha na kukuza dhamiri nyofu, ili kusaidia
mchakato wa maboresho unaopania kuifanya dunia kuwa kweli ni mahali pazuri zaidi pa
kuishi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.