Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu ni changamoto inayoitaka Jamii kuhakikisha
kwamba, inajifunga kibwebwe kungo'a mambo yote yanayopelekea ubaguzi na utengano katika
jamii. Ni ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Siku
ya kwanza ya kupambana na biashara haramu ya binadamu itakayoadhimishwa, Jumapili
tarehe 8 Februari 2015 sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, Mtawa
wa Shirika ya Wakanosaa, aliyekombolewa kutoka utumwani na hatimaye, akaongoka na
kuwa Mtawa, akajisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu waliokuwa wamekumbwa na athari
za vita nchini Italia.
Hili ni tukio ambalo limeandaliwa na Baraza la Kipapa
la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, Baraza la
Kipapa la haki na amani pamoja na Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi
za Kitume Duniani. Changamoto kubwa kwa sasa ni kung'oa umaskini na ubaguzi; mambo
yanayopelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hii ni
changamoto ya kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya uchumi na maendeleo inatoa kipaumbele
cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada
linabainisha kwamba, bado kuna umati mkubwa wa watu wanaoteseka na kuelemewa na umaskini
wa hali na kipato; kuna sera za ubaguzi wa rangi na nyanyaso za kijinsia; licha ya
harakati za jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kwamba, watoto wanapata fursa ya kwenda
shule, lakini bado kuna mamillioni ya watoto ambao hawana nafasi ya kuendelea na masomo
na matokeo yake wanajikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu, utumwa
mamboleo na kazi za suluba. Kuna magonjwa yanayotokana na afya ya akili; matumizi
haramu ya dawa za kulevya; mambo ambayo kimsingi yanachagia kwa baadhi ya watu kutengwa
na jamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema kwamba, hapa kuna haja
ya kuwa na sheria na kanuni zinazotekelezeka katika medani mbali mbali za maisha ya
binadamu, kwa kuwafikisha wahusika kwenye mkondo wa sheria na wahanga kusaidia tena
kuanza ukurasa mpya katika maisha. Kuna umuhimu kwa Jamii kubadilishana mawazo, habari
na takwimu, ili kujionea wenywewe athari na madhara ya biashara haramu ya binadamu
na utumwa mamboleo.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaungana na Baba Mtakatifu
Francisko kuwapongeza na kuwashukuru watawa wa Mashirika mbali mbali wanaoendelea
kujisadaka kwa ajili ya kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia wahanga wa biashara haramu
ya binadamu na kwamba, hata wanasiasa na watunga sheria wanapaswa kutekeleza dhamana
na wajibu wao, ili kutokomeza kabisa biashara haramu ya binadamu ambayo kimsingi ni
uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.