2015-02-06 08:46:53

Karibu sana Parokiani kwetu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 8 Februari 2015, anatarajiwa kutembelea na hatimaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya San Michele Archangelo iliyoko Pietralata, Jimbo kuu la Roma. Atakapowasili, Baba Mtakatifu atapata fursa ya kukutana na kuzungumza na wagonjwa, wazazi, walezi na wasimamizi wa watoto waliobatizwa katika miezi ya hivi karibuni.

Itakuwa ni fursa pia kwa watoto waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza kuweza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ana kwa ana. Vijana wa Skauti, wakiwa wameandamana na wazazi wao, pia watapata nafasi ya kukutana na Baba Mtakatifu, ambaye kabla ya kuanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atakwenda kwenye Kiti cha maungamo, ili kuwaungamisha waamini, tayari kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Mwaka wa B wa Kanisa.

Kama sehemu ya maandalizi ya hija hii ya Baba Mtakatifu Francisko Parokiani hapo, Monsinyo Aristide Sana, Paroko anasema kwamba, wamekuwa wakisoma na kutafakari Nyaraka mbali mbali zilizoandikwa na Baba Mtakatifu, lakini kwa namna ya pekee Waraka wa Injili ya Furaha, Evangelii gaudium; tafakari inayohitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu na Sala kwa Bikira Maria, nyota ya Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu anatarajiwa kujibu maswali na udadisi wa watoto wadogo Parokiani hapo.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1963 Mwenyeheri Papa Paulo VI alitembmelea Parokiani hapo na mwaka 1991, Mtakatifu Yohane Paulo II akaitembelea Parokia na kwa sasa wanamsubiri Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ushuhuda wa imani tendaji, inayowathamini na kuwakumbatia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni hazina na amana ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.