2015-02-06 08:38:31

Hawana nafasi tena katika Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko ameyaandikia barua Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuonya kwamba, hakuna nafasi tena kwa viongozi wa Kanisa watakaobainika wanajihusisha na vitendo vya unyanyasi wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Barua hii ni mwendelezo wa juhudi za Kanisa kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa kuunda Tume ya Kipapa kwa ajili ya kutetea watoto wadogo, tume ambayo kwa mara ya kwanza tarehe 6 Februari 2015 imeanza kukutana mjini Vatican. Tume hii iliundwa na Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Machi 2014, kwa lengo la kusaidia kutoa ushauri, mapendekezo, kanuni na sheria zitakazosaidia kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Ili kuiwezesha Tume hii ya Kipapa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, Baba Mtakatifu amewateuwa watalaam na wakereketwa wa nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu katika barua yake kwa viongozi wakuu wa Kanisa anawataka kusimama kidete, ili kuhakihakisha kwamba, madonda ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa yanakomeshwa na hatimaye, kuanza mchakato wa upatanisho na uponyaji kwa wale wote waliofikwa na mkasa huu.

Hii ni Tume ambayo ina wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, Baba Mtakatifu mwenyewe anasema, ameshuhudia machungu ya moyo kwa watu waliofikwa na mkasa wa kunyanyaswa kijinsia, lakini pia ni watu ambao wana imani thabiti, licha madonda ya ndani yanayowaandama.

Baba Mtakatifu anapenda kukumbusha kwamba, Kanisa litaendelea kubainisha mbinu na mikakati ya kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndiyo maana, Tume hii ya Kipapa inatarajiwa kuwa ni chombo madhubuti kwa Kanisa katika mchakato wa kupambana na nyanyaso za kijinsi dhidi ya watoto wadogo, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatoa haki na kuonesha huruma kwa wale wote wanaofikwa na mkasa huu.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuzihakikishia familia kwamba, Kanisa linapenda kulinda na kuwapatia watoto mazingira bora zaidi ya makuzi na kwamba, wasisite kuliendea kwa imani na matumaini. Hakuna nafasi tena ya "viongozi wa Kanisa kulindana" ili kuepuka kashfa ya nyanyaso za kijinsia, kwani viongozi wanaojihusisha na vitendo hivi vichafu hawana tena nafasi katika maisha na utume wa Kanisa.

Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na maadili vinafuatwa kwa umakini mkubwa, kwa njia ya utekelezaji wa barua ya wazi iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kunako mwaka 2011. Ni wajibu wa Mabaraza ya JMaaskofu Katoliki, kuandaa mbinu na mikakati ili kukabiliana na kashfa za nyanyaso za kijinsia.

Ni vyema ikiwa kama Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yataanzisha chombo cha kuratibu na kufuatilia sheria na kanuni zilizobainishwa. Ni wajibu wa Maaskofu pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuhakikisha kwamba, yanaunda mazingira salama kwa watoto na watu wazima wanaoweza kutumbukizwa kwenye kishawishi cha nyanyaso za kijinsia.

Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajiwekea utaratibu wa kuwahudumia wahanga wa nyanyaso za kijinsia: kisaikolojia na katika maisha ya kiroho; viongozi wawe pia na ujasiri wa kukutana na wahanga pamoja na familia zao. Huu ni muda muafaka wa kusikiliza na kuomba msamaha kwa wale waliotumbukizwa katika kashfa hizi.

Baba Mtakatifu anayaalika Mabaraza ya Maaskofu katoliki pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuhakikisha kwamba, yanashirikiana kwa dhati na Tume ya Kipapa ya kutetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Tume hii ni msaada mkubwa kwa viongozi wa Kanisa, kwa kubadilishana habari sanjari na kuendeleza mchakato wa elimu, majiundo na uhamasishaji unaoweza kutoa majibu muafaka dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha barua yake kwa Maaskofu na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa kumwomba Bikira Maria, Mama mpole na mwingi wa huruma, alisaidie Kanisa kutekeleza wajibu huu kwa ukarimu, kwa kutambua dhamana yake, tayari kulipia gharama za ukosefu wa haki kwa kashfa zilizojitokeza huko nyuma, daima Kanisa liendelee kuwa aminifu, kwa kuwalinda wale ambao Yesu mwenyewe alipenda kuwapatia kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.