2015-02-05 10:02:21

Ugaidi!


Tanzania imesema kuwa dhamira yake ya kufungua balozi katika baadhi ya nchi duniani iko pale pale na itatekeleza mpango wake huo kwa kadri hali ya fedha na uchumi inavyoruhusu. Aidha, Tanzania imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Iran katika kupambana na kukabiliana na ugaidi duniani kwa sababu nchi mbili hizo, kama ilivyo dunia nzima, zinahitaji dunia tulivu na inayosaka maendeleo ya watu bila usumbufu na matishio ya ugaidi.

Mambo hayo mawili yamejadiliwa Jumatano, Februari 4, 2015 katika mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Mheshimiwa Javad Zarif.

Mheshimiwa Zarif amewasili nchini Tanzania, Jumatano, akitokea Burundi katika ziara ambayo pia imemfikisha Kenya, Uganda na Rwanda akifuatana na maofisa wa Serikali na kundi kubwa la wafanyabiashara wa Iran. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Zarif kuwa Tanzania bado inakusudia kufungua ubalozi mjini Teheran, mji mkuu wa Iran, kama ilivyoahidi na kuwa itafanya hivyo hali ya kifedha na kiuchumi itakaporuhusu. Rais ametoa maelezo hayo kufuatia ombi la Waziri Zarif kukumbushia umuhimu wa kuwepo kwa ubalozi wa Tanzania katika Iran.

“Tunakusudia kufungua balozi katika nchi marafiki ambako kwa sasa hakuna balozi ikiwamo Jamhuri ya Kiislam ya Iran. Katika Afrika, kwa mfano, tunapanga kufungua balozi katika nchi ya: Namibia, Angola, Algeria na Ghana. Hizi ni nchi rafiki ambazo baadhi yake zimekuwa na balozi katika Tanzania tokea uhuru wetu. Mbali na Iran katika Asia, tunaangalia nchi kama Uturuki, Qatar na Kuwait na nchi nyingine marafiki,” Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Zarif.

Kuhusu mapambano dhidi ya magaidi, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Tanzania na Iran kuwa na msimamo ulio sawa wa jinsi ya kukabiliana na ugaidi. “Wakati wote, sote tunakabiliwa na matishio ya ugaidi na hivyo tunalazimika wakati wote kuwa macho na uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi. Sisi Tanzania bado tunakumbuka shambulio dhidi ya Ubalozi wa Marekani hapa nchini. Ulishambuliwa Ubalozi wa Marekani lakini watu wote waliopoteza maisha yao ni Watanzania.”

Rais Kikwete na Mheshimiwa Zarif pia wamejadili jinsi gani Tanzania na Iran zinavyoweza kuongeza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika maeneo mbali mbali ya uchumi na Rais Kikwete amemweleza Waziri fursa zilizoko katika sekta za nishati na reli. Waziri Zarif pia amemkumbusha Rais Kikwete mwaliko wa kumwomba Rais Kikwete kutembelea Iran kwa ziara ya Kiserikali.








All the contents on this site are copyrighted ©.