2015-02-05 15:15:05

Papa akutana na Maaskofu Katoliki wa Ugriki


Baba Mtakatifu Francisko Mapema Alhamisi amekutana na kundi la Maaskofu Katoliki kutoka Ugriki, waliomtembelea kama sehemu ya hija yao ya kitume katika Ofisi za Kiti Kitakatifu na Idara za Vatican kwa ujumla.
Hotuba ya Papa kwa Maaskofu hao imeanza na salaam za upendo wa kibaba akisema, hija yao katika makaburi ya Mitume, daima ni tukio maalum lenye kuimarisha uhusiano wa ushirika na Halifa wa Mtume Petro na dekania nzima ya Maaskofu, waliotawanyika kote duniani.

Umoja huu wenye kukuza ushirika wa kidugu kati yao, ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa Kanisa nchini Ugiriki, kama ilivyo pia kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Na kwa nchi yao ni hitaji muhimu zaidi, kwa ajili ya ufanikishaji mazungumzo, kati ya vyama na taasisi mbalimbali na hasa vya kisiasa, itikadi na utamaduni, kwa ajili ya ulinzi na udumishaji wa maendeleo kwa manufaa ya wote.
Papa amewataka Maaskofu wasisahau kuwaombea watu waliokabidhiwa katika huduma yao ya kiaskofu, na kuwa shahidi jasiri wa udugu, mahali popote walipo.

Papa aliendelea kuuzungumzia udugu katika dekania ya Maaskofu akisema, kwa upande mmoja inadai ulinzi na uimarishaji wa mila za kijadi na mizizi ya Kikristo ya jamii ya Kigiriki, na kwa upande mwingine inadai kujifunua kwa uwazi zaidi katika maadili ya kitamaduni na kiroho, yanayoletwa na wahamiaji wengi, katika roho ya kweli ya kuwakaribisha ndugu hawa, wake kwa waume bila ya ubaguzi wa rangi, lugha au dini. Papa amesihi, jamii yao ya Kikristo, ionyeshe kweli umoja kati yao na wakati huo huo kufungua njia za kukutana na kuwapokea, hasa wahamiaji walio katika hali ngumu zaidi, ambao wanaweza kutoa mchango wao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii, sambamba mafundisho ya Injili.

Papa alionyesha kufurahia kwamba, tayari Maaskofu wanashiriki katika shughuli hii kupitia kazi zao za kichungaji na hisani, hasa kwa ajili ya wahamiaji, ambao wengi wao ni Wakatoliki. Kwa moyo wake wote Papa amewahimiza Maaskofu waendelee na jitihada mpya za kimisionari, na hasa kwa kuwashirikisha zaidi vijana: ambao ni mustakabali wa taifa.

Papa aliendelea kuzungumzia changamoto za uchumi na fedha zinazowakabiliwa, kama ilivyo sehemu nyingine za dunia, na kuwataka wasichoke wala kukata tamaa katika kujenga tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Na wawe na ujasiri wa kupambana kile kinachojulikana kama utamaduni rajua, kuona kwamba mambo yote ni mabaya. Papa amehimiza moyo wa mshikamano ambao Wakristo wote wanatakiwa kuuishi na kuushuhudia katika hali halisi ya maisha ya kila siku, kama chachu ya mshikamano na matumaini.

Amesema, Ni muhimu kwamba, kila Askofu anadumisha uhusiano wake wa karibu na utawala wa nchi, ikiwa ni pamoja na taasisi na vyama mbalimbali vya jamii, ili kueneza moyo wa umoja na mshikamano, kupitia njia ya majadiliano na kushirikiana na nchi nyingine za Ulaya.
Katika roho hiyo, Papa pia amewahimiza waendelee na mazungumzo ya ana kwa ana na Waotodosi, katika kuilisha safari muhimu ya kiekumeni na matarajio mazuri katika utulivu na mafanikio ya kiroho kwa manufaa yao wote.

Papa pia hakuchelea kuzungumzia utekelezaji wa utume wa Uinjilishaji na kukuza ubinadamu kama wito wa Kanisa nchini Ugiriki, na huduma isiyokwepeka katika ukarimu na motisha ya viongozi wa dini. Kwa hiyo, aliwasihi, Maaskofu waongeze zana sahihi, huduma nzuri kitaaluma, na kushughulikia upungufu wa watumishi. Katika suala hili, aliwaomba wafikishe kwa mapadre wa majimbo yao, ambao wengi wao ni wazee, upendo wake kwa wote na shukrani zake za dhati kwa bidii yao ya kitume, licha ya ufinyu wa njia.

Papa ametaja umuhimu na thamani ya mchango wa kutangaza Injili kwa Taasisi za Maisha wakfu, na akatoa mwaliko wa kutoa angalisho makini sahihi, kwa sababu, licha ya matatizo mengi, lengo la Unjilishaji liweze kuendelezwa Ugirki. Papa alieleza huku akipeleka mawazo yake hasa katika uwanja wa elimu. Na pia katika uimarishaji wa jamii ya Kikristo, akisema wameitwa kuongeza nafasi ya waamini walei katika utendaji wa shughuli nyingi za Kanisa. Na kwamba, Ushirikiano wao na huduma ya maaskofu na makasisi inahitajika kushughulikia changamoto za leo na pia katika mtazamo wa siku zijazo.

Na hii ina maana ya kuwa na malezi mazuri ya kutosha kupitia mipango ya elimu, na pia katika lengo la kuongeza uwepo wa walei katika harakati na vyama Kanisa. Na haya yote yanahitaji maongozi mazuri ya Kichungaji, popote kuwawezesha walei kuthamini dhamira yao ya kimisionari na furaha ya kuwa Mkristo, katika kueneza na kutenda daima kwa maelewano ya pamoja na miongozo ya kichungaji kwa Makanisa maalum iliyowekwa kijimbo na katika Parokia.

Papa pia amezungumzia hoja ya kudhoofika kwa familia, ambako pia kunasababishwa na changamoto za malimwengu, na hivyo inahitaji dhamira ya Kanisa ya kudumu katika mipango ya utoaji mafunzo kwa wale wanaolenga kufunga ndoa, na hasa juu ya malezi ya vizazi mpya, kama sehemu ya malezi ya Kikristo.

Amewataka Maaskofu wasisahau kundi la wazee katika huduma yao , wazee ambao wengi wao sasa wanajikuta wameachwa katika upweke au kutelekezwa, kwa sababu kuzuka kwa utamaduni wa taka, unaozidi kupanda chati siku hadi siku kila mahali. Maaskofu wasichoke kusisitiza kwa maneno na vitendo kwamba uwepo na ushiriki wa wazee katika jamii ni muhimu kwa jamii kutembea katika njia sahihi.

Papa alikamilisha hotuba yake na shukurani za dhati kwa Maaskofu, kwa ajili ya kazi ya uinjilishaji ambayo, licha ya matatizo mengi, wanaendelea kuifanya nchini mwao Ugriki. Na akashukuru kwamba, kutambuliwa kisheria Kanisa Katoliki na serikali , ni tukio kubwa muhimu, la kuwapa nguvu na ujasiri wa kutenda kwa kujiamini zaidi kwa ajili ya ufanikishaji utendaji wa leo na pia kwa ajili ya manufaa ya siku zijazo, kwa shauku zaidi katika kuwa mashahidi wa Bwana, aliyekufa na kufufuka.

Papa amewaomba Maaskofu wajenge moyo wa kuvumilia kwa furaha ya Kiinjili. Na aliwakabidhi Mapadre, watawa na waamini wote wa kawaida wa Majimbo yao, chini ya maombezi ya Bikira Maria na, pia akaomba maombi yao kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya huduma yake kama Khalifa wa Mtume Petro, na kuwapa Baraka zake za Kitume.








All the contents on this site are copyrighted ©.