2015-02-05 09:50:15

Maaskofu kati ya Maskini!


Maaskofu 70 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaojisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kati ya Familia ya Mungu iliyohudhuria Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatano, tarehe 4 Februari 2015, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican. Hawa ni Maaskofu wanaoshiriki katika mkutano ambao umeandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma.

Akiwatambulisha Maaskofu hawa, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia, alimwambia Baba Mtakatifu kwamba, kundi hili la Maaskofu liko mjini Roma, ili kufanya hija ya pamoja inayopania kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hii ni huduma ya upendo inayomgusa na kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya mwamini; kwa kuvuka mipaka ya kudhaniana vibaya, tayari kuanza mchakato wa urafiki na udugu.

Maaskofu wanatambua kwamba, katika maisha na huduma yao, wanaliwakilisha Kanisa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anawatuma watoto wake kuzingatia haki na kutenda mema, ili waweze kupata maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.