Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACEAC, linalounganisha
Maaskofu kutoka DRC, Rwanda na Burundi, katika mkutano wao wa mwanzo wa mwaka wamejadili
na kukazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Familia ya Mungu kusimama kidete kulinda
na kutetea tunu msingi za maisha ya familia; ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji sanjari
na ujenzi wa misingi ya haki na amani. Hizi ni kati ya changamoto zinazofanyiwa kazi
na Kanisa huko Afrika ya Kati.
Ujumbe uliotolewa na Maaskofu baada ya mkutano
huu, unawahimiza waamini kushuhudia Injili, kwa kumwilisha imani katika uhalisia wa
maisha, huku wakiendelea kuwashirikisha jirani zao, tunu msingi za maisha ya Kikristo
na utu wema; mambo ambayo kwa sasa hayana budi kupewa kipaumbele cha pekee. Kanisa
katika maisha na utume wake, linapenda kuwa ni chumvi na mwanga wa dunia, hasa wakati
huu ambapo kuna pilika pilika za mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
mwaka huu nchini Burundi.
Kuna baadhi ya wanasiasa wanataka kuhakikisha kwamba,
wanaingia madarakani kwa nguvu zote, hata ikibidi, kumwaga damu! Jambo ambalo Maaskofu
wanasema, haliwezi kukubalika, kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi
mema, kuendelea kujikita katika misingi ya haki, amani na demokrasia ya kweli, huku
wakiombea amani na utulvu, ili demokrasia ya kweli iweze kushika mkondo wake.
Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, linapenda kuwasindikiza wanasiasa
katika utekelezaji wa mikakati na sera za maendeleo na uchumi kwa kujikita katika
mchakato wa haki, amani na upatanisho katika eneo la Maziwa Makuu. Maaskofu bado wanaendesha
kampeni ya amani katika eneo la Maziwa Makuu, kampeni ambayo ilizinduliwa kunako mwaka
2013, kwa lengo la kushuhudia imani kwa Yesu Kristo, Mfalme wa amani; sanjari na kuwajengea
wananchi uwezo wa mfungamano wa kijamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mchakato
wa amani, badala ya kutumia mtutu wa bunduki.
Ni wajibu wa Familia ya Mungu,
kutoka katika eneo la Maziwa Makuu, kuhakikisha kwamba, inajielekeza katika ushuhuda
wa maisha unaopania kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili inayofumbatwa
katika utamaduni wa haki na amani.
Maaskofu wanasema kwamba, mchakato wa Uinjilishaji
mpya sanjari na familia ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa katika
eneo la Maziwa Makuu. Maaskofu wanaendelea kutafakari kuhusu matatizo, changamoto
na fursa mbali mbali ambazo familia nyingi zinakabiliana nazo, ili kuweza kutoa majibu
muafaka na kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia
itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2015.
Maaskofu wanasema, kuna haja
ya kuonesha ushirikiano na mshikamano wa dhati miongoni mwa nchi za Maziwa Makuu,
katika harakati za kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, dhamana inayoweza
kuratibiwa kwa njia ya Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, yaani Caritas katika
nchi husika. Mwishoni, Maaskofu wametembelea kwenye eneo la Kumbu kumbu ya Kabgay,
ili kutoa heshima zao kwa wale wote waliopoteza maisha yao wakati wa mauaji ya kimbari
yaliyofanyika nchini Rwanda kunako mwaka 1994.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.