Askofu mkuu Telesphore Mpundu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia anamwomba
Rais Egdar Lungu na Serikali yake kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa
na ujenzi wa Zambia kwani sasa pilika pilika za kampeni na hatimaye uchaguzi zimekamilika
na uongozi unapaswa kuanza kutekeleza dhamana na majukumu yake barabara.
Katika
mchakato wa upigaji kura, kila mtu alikuwa na mawazo na kiongozi wake aliyependa kumpatia
kura yake kama sehemu ya utekelezaji wa Katiba na wajibu wa kiraia, kumbe, katika
hili, taifa na wananchi wake walikuwa wamegawanyika, sasa ni wakati wa kuanza mchakato
wa uponyaji unaojikita katika moyo wa msamaha na upatanisho, ili kukoleza utamaduni
wa amani na utulvu.
Licha ya mchakato wa uchaguzi mdogo kumalizika kwa amani
na utulivu, lakini kuna kasoro ndogo ndogo ambazo hazina budi kufanyiwa kazi kwa siku
za usoni, ili kuhakikisha kwamba, Katiba ya nchi inalindwa na kuheshimiwa na wanasiasa
wote. Kuwepo na amani na utulivu katika vyama vya kisiasa kabla ya kuanza kujikita
katika kutafuta kura za wananchi ili kuongoza Taifa, kama ilivyojitokeza kwa vyama
vingi vya kisiasa nchini Zambia.
Askofu mkuu Telesphore Mpundu anawataka wanasiasa
kuhakikisha kwamba, wanatekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni, ili
kuwajengea tena watu matumaini katika ushiriki wao kwenye masuala ya demokrasia na
utawala bora. Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linasikitika kusema kwamba, kuna
baadhi ya wanasiasa wanatumia vyombo vya mawasiliano ya kijamii ili kupandikiza ukabila
badala ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa; ukabila kwa sasa hauna mguso wala
mashiko kwa watu.
Kanuni maadili za uchaguzi zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa
na wote na kwamba, viongozi wa Kanisa hawana sababu ya kujiingiza katika kampeni za
uchaguzi kwa kuonesha upendeleo, changamoto ya kuangalia mapungufu yaliyojitokeza
ili kujipanga vyema zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tena nchini
Zambia, kunako mwaka 2016. Tume huru ya uchaguzi Zambia haina budi kujengewa uwezo
ili kuboresha Daftari la Wapiga kura pamoja na vituo vya kupigia kura.
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.