2015-02-04 09:15:54

Tacloban ulikuwa ni moto wa kuotea mbali!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua ya shukrani Askofu mkuu John Du wa Jimbo kuu la Palo, Ufilippini kwa kusema kwamba, katika maisha na utume wake, hataweza kusahau kamwe Taclobani. Hapa waamini wameonesha na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na udumifu hata wakati wa shida na mahangaiko yao! Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kuwakumbuka katika sala na utume wake.

Licha ya mvua kubwa iliyokuwa inanyeesha, huku ikiandamana na upepo mkali, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa Tacloban, tarehe 17 Januari, 2015 lakini waamini walisali kwa moyo wa ibada na uchaji mkuu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwa kuona ushuhuda wa imani tendaji, alikoswa hata neno la kusema. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume nchini Ufilippini kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 19 Januari 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.