2015-02-04 09:47:53

Mediterrania: Mahali pa watu na tamaduni kukutana!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika ujumbe wake kwa kikao cha tisa cha wabunge kutoka katika nchi za Mediterrania, kilichoanza Jumatatu tarehe 2 Februari na kuhitimishwa tarehe 4 Februari 2015, anakumbusha kwamba, Mediterrania inapaswa kuwa ni mahali pa watu kukutana na kamwe isitumike kwa ajili ya vita, kinzani na chuki kwa kisingizio cha kidini.

Wajumbe wanapaswa kutoa majibu muafaka ili kukabiliana na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama na ubora wa maisha Barani Ulaya; makundi ambayo kwa bahati mbaya yanatumbukia mikononi mwa watu ambao dhamiri zao zimekufa na matokeo yake, ni kuwasukumiza katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko anasema Kardinali Parolin kwamba, wajumbe wataweza kuibua mbinu mkakati utakaosaidia ujenzi wa mchakato wa watu kukutana katika Ukanda wa Mediterrania. Kwa sasa nchini hizi zinakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kinzani za kisiasa kutoka katika baadhi ya nchi za Kiafrika, vita na vitendo vya kigaidi huko Syria na Iraq.

Inasikitisha kuona kwamba, katika kipindi cha mwaka 2014 vitendo vya kigaidi vimeongezeka maradufu kiasi cha kutishia usalama, amani na haki msingi za binadamu. Vatican kwa upande wake inahofia usalama na maisha ya Wakristo huko Mashariki ya Kati pamoja na kutambua kwamba, kuna Waislam ambao pia wanateseka na kunyanyasika kutoka kwa waamini wenye misimamo mikali ya kiimani.

Lakini ikumbukwe kwamba, kamwe, vita kwa kutumia jina la Mungu haviwezi kuhalalishwa kama anavyokemea Baba Mtakatifu Francisko. Vitendo hivi havina budi kukemewa na kulaaniwa kwa "macho makavu bila kusita" hata na viongozi wa dini ya Kiislam. Kwa miaka mingi Mediterrania imekuwa ni eneo la makutano kati ya watu na tamaduni mbali mbali, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, eneo hili linaendelea kuwa ni uwanja wa watu na tamaduni kukutana, kwa amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.