2015-02-03 14:28:31

Tumbo moto!


Homa ni ugonjwa wa ajabu unaolegeza viungo vya mwili kutokana na kupanda na kushuka kwa joto mwilini. Kadhalika homa inamnyima mgonjwa hamu ya kula. Mapato yake homa inamdhoofisha na kumkosesha nguvu na kumlaza kitandani na mgonjwa hawezi kufanya shughuli yoyote ile.

Kwa kiswahili cha mitaani, neno “homa” linatumika kumaanisha woga wa kukabili maisha, mathalani hali ya kuogopa mitihani wanaita “homa ya mitihani” au yamaanisha pia udhaifu au tabia mbaya inayoweza kumkumba mtu au hata kuikumba jamii fulani wanaita “homa ya jiji, homa ya kijiji, homa ya vijana, homa ya Kanisa, homa ya Wakristo, homa ya watawa, homa ya mapadre, homa ya mabunge wetu, nk, wakimaanisha kasoro au tabia fulani mbovu inayoinasa na kuipagawaza jamii hadi jamii nzima ikajisikia inaumwa nayo bila kujitambua.

Kwa mfano tunaweza pia kusema rushwa ni “homa ya nchi,” au tabia ya kuiga mitindo ya maisha ya mataifa ya ulaya au Amerika, hiyo ni “homa ya Waafrika.” Homa za mtindo huo zinaweza kuwadhoofisha watu wote hata viongozi wa serikali na dini hadi wanalazwa kitandani na kushindwa kufanya kazi ya haki, upendo na amani. Aidha ni ngumu sana kupona toka homa aina hizo.

Hebu leo tumfuatilie kwa makini mwalimu, mwanamapinduzi anavyomnusuru mtu mwenye kunaswa na homa kali hadi kumlaza kitandani, na baada ya kupona anaendelea na shughuli zake za kawaida. Kituko cha leo ni kifupi sana ukikilinganisha na vituko vingine vilivyoelezwa katika injili. Lakini kinavyoelezwa, hakimaanishi kutupatia taarifa au maarifa ya kiakili, bali kipo kwa ajili ya kutupatia ujumbe mkuu wa maisha yaani ni kama katekisimu. Mwinjili anataka kutuonesha mabadiliko, au mapinduzi yaliyoweza kupatikana ulimwenguni hapa baada ya Yesu kuingia duniani.

Tulishasikia kwamba ilikuwa ni siku ya Jumamosi (Sabato) Yesu alikwenda kwenye Sinagogi kufanya ibada. Kule Sinagogini tulikishuhudia kizungumkuti cha mtu mwenye mapepo. Mara baada ya ibada hiyo ya Jumamosi Yesu akatoka na wanafuasi wake Petro na Andrea wakitanguzana pia na Yakobo na Yohane waliokuwa wameitwa kumfuata wakarudi kuelekea nyumbani kwa Petro palepale kijijini Kafarnaum.

Wanapofika nyumbani kwa Petro na Andrea, wafuasi hawa wanamkuta mamamkwe yaani mama ya mke wa Petro anayo homa na amelala hoi kitanda hajiwezi. Mara moja wafuasi hawa wanamtaarifu Yesu. Kitendo hiki cha wafuasi kuchukua jukumu la kumtaarifu Yesu, kinatufundisha kuwajibika tunapoona ndugu au jirani anaumwa.

Kwa hiyo yasemwa: “Mkwewe simoni mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa,” maana yake amelala kitandani na hawezi kufanya chochote, hawezi kuamka na kushughulika na kazi ya kujenga familia au taifa. Amefungwa, amezuiliwa na hawezi kuwa mtu kamili na kufanya anachotakiwa mtu mwenye afya kukifanya. Homa hii haijulikani imesababishwa na ugonjwa gani bali ni homa tu. Hali ya homa ya mkwe wa Petro inawakilisha ulimwengu wa kale, ulimwengu ambao siyo wa utu kamili. Sisi sote ni waana wa Mungu, na tunao uana wa kimungu ndani mwetu, lakini uana huo ukipatwa na homa haukui bali unabaki umesinyaa tu kama “Kandunji” yaani mtu aliyedumaa na asiyerefuka.

Hiyo ni homa ya maisha. Je, ni homa gani inayotudumaza, inayotulaza kitandani tusiweze kuinuka, tusiweze kuwa watu na watoto halisi wenye sura ya Mungu? Homa hii inayotupooza kabisa ndiyo ubinafsi, yaani kujifikiria mwenyewe tu. Kutojali wala kuwathamini wengine. Homa inayotuzuia tusikue na kuendelea kuwa na ule uwaana wa Mungu ulio ndani mwetu ambao ni kufanya kazi ya kutumikia wengine kwa upendo.

Hebu tuone jinsi Yesu anavyoponya homa hii. Kwanza anamkaribia mgonjwa, yaani hamwogopi mwenye homa bali anamkaribia. Katika tendo hilo la kukaribia sisi tunapata ujumbe muhimu, yaani kule kumkaribia mgonjwa kwaonesha kuthamini na kugundua hali inavyomnyima jirani na jamii utu stahiki. Hali halisi ya ulimwengu haijali utu, yaani homa ya ulimwengu, kama vile umaskini, maradhi, vita, unyanyasaji, rushwa, wongo, nk. Sisi hatuikabili homa hiyo kwa karibu. Tunatoroka tunapoona mambo hayaendi inavyotakiwa.

Kumbe Yesu anapoikaribia na kuikabili homa, hapo hali inabadilika. Katika homa kama hii inayomfanya mmoja asiweze kuamka kuwa mtu kamili na kuendelea kufanya kazi haifai kujifanya hamnazo na kutoona au bila kusema kitu. Kama hakuna anayekaribia basi unaalikwa wewe mkristu kukaribia na kuikabili. Hivi hatua ya kwanza ni kuikabili hali halisi ya homa. Baada ya kumkaribia mgonjwa, Yesu anamshika mkono na kumwinua. Kwa kigiriki kuinua ni “egeirein” lenye maana ya kumwinua usingizini kama vile angekuwa mfu na kumpa tena uhai. Ama kweli mtu asiyeweza kupenda, mtu mbinafsi huyo ni mfu ni msiba unaotembea. Yaonekana kuwa mama huyu alikuwa kama mfu tu, hivi Yesu anamwinua, hapo homa inamwacha.

Mara tu baada ya kupona “anawatumikia.” Hapo maisha mapya yanaonekana katika kutumikia, katika kuwapenda wengine, na kufanya kitu kwa ajili ya jamii. Mtu amepona pale anapoanza kutumikia. Huyu sasa ni mtu mpya aliyezaliwa katika mazingira fulani anayoshindwa kupenda na sasa anakuwa tayari kumtumikia jirani hasa pale anapolitambua Neno la Mungu. Kwa hiyo mapinduzi aliyofanya Yesu hapa ni kule kumwinua mgonjwa na kumfanya aweze kutumikia ndugu zake. Tunapotaka kutumikiwa na wengine hapo tunakuwa na homa ya ubinafsi, tunakuwa wafu. Kumbe tunapotumikia wengine tunakuwa huru.

Katika kuhitimisha sehemu hii inasemwa kwamba “kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuja wagonjwa wengi na wenye pepo. Wote walikuwa wamekusanyika mlangoni.” Kusanyiko hilo linaeleweka kabisa kwa vile ilikuwa ni jumamosi jioni siku ya mapumziko na asubuhi yake walikuwa kwenye ibada ya Sinagogi. Lakini kulikoni wakusanyike mlangoni, tena basi ni mlangoni pa nyumba ya famili alimokuwa anaishi Yesu na Petro?

Hapo mlangoni, ndipo palijaa fundisho kwetu. Yaonekana mle ndani ya nyumba kulikuwa na Neno la uhai, neno linalookoa na linaloponya aina ya homa za watu wote waliokusanyika pale mlangoni. Kwa hiyo picha na fundisho unayoweza kuipata ni kwamba ulimwengu mzima unasubiri katika mlango wa nyumba inamokaa familia na jumuia yenye kutoa Neno la amani, Neno la utu, Neno la haki na Neno la upendo na heshima.

Hapa unaachiwa mwenyewe kufanya tafakari juu ya nyumba yako na jumuia yako hata dini yako, endapo watu wanakusanyika hapo na kwa lipi. Kama watu hawakusanyiki mlangoni pa nyumba ya mtu ujue wakazi wake wamehama au wamelala kitandani hawawezi homa. “Palipo na upendo na mapendo hapo Mungu yuko.”

“Alfariji na mapema sana Yesu akaondoka na kwenda kuomba.” Lengo la kuomba ni kutaka kuunganisha matendo na maneno yake na mapenzi ya Mungu Baba yake. Kwa hiyo, hata sisi tukitaka kujenga ulimwengu yabidi kulinganisha shughuli zetu katika maisha na mapendo ya Mungu.

Petro na wafuasi hawakuelewa kwa nini Yesu anaomba au anasali wakamwambia: “Watu wote wanakutafuta.” Yesu ikabidi awaambie wazi kwamba ujumbe huu unaowanasua watu toka kwenye homa zako, tusiubinafsishe na kuubana ubaki hapa Kafarnaumu, bali twendeni vijiji vingine, kwa jumuia zote za Kiyahudi, na ulimwengu wote tukatangaze Neno hili litakalomwamsha mtu kutoka “homa ya jiji” yaani ubinafsi.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.