2015-02-03 14:10:50

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Ni siku nyingine tena tunakutana kushirikishana furaha yetu itokayo katika Neno la Mungu. Ni dominika ya V ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa ametuwekea Neno linalotukumbusha mateso na masumbuko katika safari ya wokovu na jibu analotoa Bwana dhidi ya mateso haya. RealAudioMP3

Nabii Ayubu katika somo la kwanza anatufundisha kuvumilia mateso kama sehemu ya maisha yetu tunapojitahidi kumtafuta Mungu na kuishi mapenzi yake. Tuzo la uvumilivu wetu katika mahangaiko haya tunaalikwa kulipata baadaye tutakapokuwa tumemalizia safari yetu vizuri ya maisha ya kikristu na hivi kuurithi uzima wa milele.
Daima jambo la kuteseka katika maisha ya mwanadamu ni jambo ambalo watu hujiuliza na kuliwekea mashaka na kusema, kwa nini kuna mateso?

Je, Mungu yuko wapi? Kwa nini kuna vita, matetemeko, uvamizi, na njaa katika nchi yetu? Utasikia hata wakati fulani watu wakisema kwanini nilizaliwa? Kwa hakika jibu la moja kwa moja hatujaweza kulipata lakini twaweza kujifunza kitu toka Mama Bikira Maria katika agano jipya.

Kama tulivyosikia katika injili iliyosomwa ktk sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu Januari mosi mwinjili anatuambia “akayaweka yote moyoni” yaani anatarajia mapenzi ya Mungu yafanyike. Anamwona Mungu katika yote, hivi nasi leo katika mateso na magumu tumwone Mungu anayetupenda, anayetualika kuvumilia kama Mwanae alivyovumilia pale msalabani na matunda yake ni kutujalia wokovu.

Ni katika kuvumilia mateso Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto katika barua yake ya I sura ya tisa anatualika kuhubiri habari njema kwa bidii na ustadi kwa watu wote na kwa furaha. Anatangaza ole kama mmoja wetu hatahubiri injili, kwa maana tumepokea wajibu huo kwa njia ya ubatizo. Hata hivyo katika kuhubiri habari njema tunapaswa kutafuta daima si mastahili yetu bali mastahili ya msalaba wa Kristo.

Injili yapaswa kupelekwa bila gharama, yaani mmoja asiweke visingizio ambavyo vyaonesha uvivu na majikwezo yaani kujiweka katikakati kama kitovu cha shughuli nzima ya wokovu wa watu badala ya kumtanguliza Kristu nyota angavu inayoongoza historia na ulimwengu.

Mwinjili Marko anatuonesha ni namna gani Bwana wetu Yesu Kristu anatoa jibu dhidi ya mateso. Anamponya mama mkwe wa Simoni Petro aliyekuwa mgonjwa. Ndiyo kusema kama kuna mmoja wetu anateseka yatupasa kutoa msaada unaohitajika na kwa namna hiyo tutakuwa tunatoa polepole jibu dhidi ya mateso ya mwanadamu badala ya kuendelea kujiuliza kwa nini kuna mateso duniani.

Bwana anawapa moyo Wamisionari kuwa wasiwe na hofu juu ya familia zao, yeye mwenyewe atazitunza na kuzijalia furaha, atakuwa nao wakati wa taabu. Zaidi ya Mama mkwe wa Mt. Petro, Bwana anaendelea kuwaponya wagonjwa wengine, akitupa picha yakuwa yeye ni kwa ajili ya wote, ni mganga na mchungaji mwema.

Leo hii tunaalikwa kuwahudumia watu wote wenye shida mbalimbali bila ubaguzi. Anapotoa huduma hasahau kujikusanyia nguvu na hivi anajipatia muda wa kusali. Wakristu daima husali ili kupata nguvu ya kukabiliana na mateso katika maisha yao.
Mpendwa, mara kadhaa tunakwepa kuwajibika na hivi matatizo husonga mbele katika jumuiya zetu.

Kumbe tuige mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo anapomshika mkono Mama mkwe wa Mt Petro na kumnyanyua juu aonesha tendo la ufufuko toka taabu ya magonjwa na hivi mkono wa Bwana ni ufufuko kwa walio katika kifo cha dhambi, umaskini na ugonjwa. Aonesha kuwa Mungu hapendezwi na magonjwa bali apendezwa na ustawi wa watu wake. Wajibu wetu leo pengine si miujiza bali kufuata mafundisho ya Bwana na hivi kupendana kina na kwa njia hiyo tutakomesha vita, njaa na magonjwa mengine hapa duniani.

Nikutakieni furaha daima pamoja na uwajibikaji ukitafakari Neno la Mungu daima.
Niseme tukutane tena muda na wakati kama huu Dominika ijayo. Pd R. Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.