Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, kwa kuwahimiza watawa
kuwa kweli ni mashuhuda wa Furaha ya Injili na Manabii wanaowatangazia Watu wa Mataifa
matendo makuu ya Mungu kwa njia ya huduma makini mintarafu karama za Mashirika ya
kitawa na kazi za kitume.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuyapyaisha
maisha na utume wao kwa kuonesha utii na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, tayari
kujisadaka kwa ajili ya kuwaamsha walimwengu, kwa njia ya Uinjilishaji mpya.
Kardinali
Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za
kitume anasema, Baba Mtakatifu anapenda kuwashirikisha watawa ile furaha ya kweli
inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu na changamoto zinazojitokeza
katika maisha na utume wao, hususan katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya
sayansi na teknolojia.
Maisha ya kitawa na kazi za kitume ni sehemu ya mchakato
wa mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene, ili kuwawezesha Wakristo wa Makanisa na
Madhehebu mbali mbali kumshuhudia Kristo, kwa njia ya sala, huduma na majadiliano
ya kina, cheche ambazo Kardinali Joao Braz di Aviz anasema, zimejionesha kwa mara
ya kwanza wakati wa maadhimisho ya Juma la kuombea umoja wa Wakristo sanjari na maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa.
Hii ni changamoto kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko
anayewahamasisha waamini kujenga madaraja na utamaduni wa kukutana, kupendana na kusaidiana,
ili kuweza kushirikishana uzoefu na mang'amuzi ya uwepo wa Mungu kati yao! Makanisa
ya Mashariki na Watawa wao, wana utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho; mambo ambayo
watawa wanaweza kushirikishana kama sehemu ya mchakato wa kutajirishana, kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa
katika maisha ya kitawa na kazi za kitume, yalenge kukoleza moyo wa kufuasa Kristo
zaidi, ili kumshuhudia kati ya Watu wa Mataifa; kwa kuendelea kujikita katika toba
na wongofu wa ndani, sanjari na kusoma alama za nyakati.
Kuna umati mkubwa
wa watawa wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, lakini kwa masikitiko
makubwa, Baba Mtakatifu anashangaa kuona jinsi ambavyo kila mwaka kuna watawa wa kike
na kiume wanaoamua "kubwaga manyanga" na kuanza maisha mapya. Takwimu zinaonesha kwamba,
kuna watawa zaidi ya millioni moja na nusu wanaoishi na kufanya kazi na utume wao
katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume elfu tatu!
Kumbe, inasikitisha
kuona watawa wakiacha wito wao na kuamua kufuata njia nyingine ya maisha! Hapa kuna
haja ya kufanya tafakari ya kina, ili kuboresha hali ya maisha inayowatatiza watawa,
ili hatimaye, waweze kujisikia kweli wako nyumbani na kuendelea kudumu hadi pale Mwenyezi
Mungu atakapowaita kutoka katika dunia hii!.
Baba Mtakatifu anawaalika watawa
kuangalia mambo makuu matatu: mang'amuzi ya maisha na wito wa kitawa, jambo ambalo
linapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kutambua lengo kuu linalomsukuma kijana
kuacha yote kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Pale maamuzi na malengo yanaposigana,
si haba kuona kwamba, watu wanaamua kuacha wito na maisha ya kitawa.
Hatua
ya pili muhimu ni majiundo makini ya awali na endelevu; hapa ikumbukwe kwamba, watawa
wanafundwa si tu na mtu mmoja ambaye ameteuliwa kuwa ni mlezi, bali jumuiya na mahali
ambapo malezi haya yanafanyika bila kusahau athari za jamii inayowazunguka. Watawa
wanapaswa kutambua kwamba, daima wao ni sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu, hadi
pale watakapoingia kaburini.
Majiundo makini yalenge kuwasaidia watawa kumfuasa
Kristo: fukara, mseja na mtii, kwa kujikita katika karama za waanzilishi wa Mashirika
yao, tayari kusoma alama za nyakati ili kuzipyaisha na kuzimwilisha katika uhalisia
wa watu wanaowahudumia kwa sasa.
Baba Mtakatifu anasema, hatua ya tatu ni ile
inayopasa kumwangalia mtawa kama sehemu ya fumbo la maisha ya mwanadamu; mwanadamu
ataendelea kubaki kuwa ni fumbo kwake mwenyewe na hata kwa wale watu wanaomzunguka,
ndiyo maana kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana katika ukweli
na uwazi, ili kulifahamu fumbo la maisha ya mwanadamu!
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.