Bwana Sergio Mattarella, baada ya kula kiapo cha utii kwa Katiba ya Nchi, kuhutubia
Bunge na Taifa kwa ujumla, akapigiwa mizinga ishirini na moja pamoja na kutembelea
Altare ya wahenga wa Italia, kuanzia tarehe 3 Februari 2015 anakuwa ni Rais wa kumi
na mbili wa Italia.
Katika hotuba yeke ya kwanza kama Rais wa Italia, amekazia
kwa namna ya pekee umoja na mshikamano wa kitaifa ili kupambana na ukosefu wa haki,
umaskini na upweke ili kuanza mchakato wa kuwajengea wananchi wa Italia matumaini
mapya, kwa kuwapatia haki na huduma msingi za kijamii. Kuna kundi kubwa la vijana
wasiokuwa na fursa za ajira, hawa wanapaswa kusaidiwa, ili kuwa na matumaini ya leo
na kesho iliyo bora zaidi kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya uchumi.
Rais
Mattarella anawataka wafanyakazi wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia
misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu na uwajibikaji; makini katika maneno na matendo
yao. Ametaka wanasiasa kufanya mabadiliko ya kweli katika uwanja wa kisiasa, kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya taifa na kwamba, uongozi ni huduma sanjari na kuendeleza
mchakato wa mabadiliko ya Katiba ili kuimarisha demokrasia. Kama Rais atasimamia,
kulinda na kutetea Katiba ya Nchi.
Rais Mattarella anamshukuru Baba Mtakatifu
Francisko kwa ujumbe wa matashi mema aliyomwandikia hivi karibuni, anaungana naye
kulaani rushwa na ufisadi wa mali ya umma; ukosefu wa haki, amani na utulivu na kwamba,
kwa sasa vitendo vya kigaidi vinatishia usalama na mfungamano wa kijamii katika ngazi
mbali mbali. Hapa kuna haja ya kuachana na tabia ya chuki na kupenda kulipizana kisasi;
mambo ambayo yameigharimu Italia kwa kiasi kikubwa.
Rais Mattarella anaitaka
Jumuiya ya Kimataifa kuvalia njuga tatizo la vitendo vya kigaidi, ili kuwahakikishia
watu usalama wa maisha na mali zao; amani na matumaini. Anasema vita kwa malengo yoyote
yale, haina tena mashiko wala mvuto bali itaendelea kusababisha majanga, kumbe kuna
haja ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Italia
itaendelea kushirikiana kwa hali na mali katika mahusiano ya kimataifa na kwa namna
ya pekee kabisa amemkumbuka Padre Paolo Dall'Oglio na wengine ambao wametekwa nyara
na hadi sasa hawajulikani mahali walipo. Watu wanataka kuwa huru, kwa kuishi katika
amani na mshikamano; watu wanaojisiia kuwa kweli ni Jumuiya inayojikita katika mchakato
wa ujenzi wa matumaini mapya.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.