2015-02-03 09:49:29

Hoja msingi ni huduma!


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Jumatatu tarehe 2 Februari 2015 amekutana na kuzungumza na mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama mwanzo wa utume wake. Amewatakia wote ushirikiano, ustawi na maendeleo kwa wote. RealAudioMP3

Kuwa mwakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia si utume wa kujivunia, kwani jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni wito wa Kipadre, kwani amewekwa wakfu kwa ajili ya kuwagawia Watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa na kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Padre au Askofu akiwa na mwelekeo kama huu anaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa moyo mkuu na mnyofu, kwa ajili ya sifa na utuku wa Mungu pamoja na Kanisa.

Ni maneno ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu anapojiandaa kutekeleza utume wake mpya hapa mjini Vatican. Alianza shughuli zake za kidiplomasia nchini Tanzania na kuhitimisha huko nchini Australia.

Askofu mkuu Gallagher anasema, kwa sasa dunia inakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto kubwa zinazojikita katika mikakati ya maendeleo endelevu inayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Katika shida na mahangaiko yao, watu wanaonesha cheche za matumaini kwa dunia iliyo bora zaidi, licha ya kinzani, migogoro na vita kuendelea kutikisa misingi ya maisha ya watu wengi duniani.

Lakini ikumbukwe kwamba, umaskini, ujinga na maradhi ni matokeo ya vita, uchu wa mali na madaraka pamoja na kutozingatia kanuni maadili ya kazi. Kwa mwelekeo wa namna hii, watu wanakatishwa tamaa na kujikuta wametumbukia katika kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kuhatarisha maisha ya watu wengu duniani.

Askofu mkuu Gallagher anasema, katika maisha na utume wake kama Mwanadiplomasia wa Vatican amekutana na upinzani kutoka katika kundi dogo la watu ambao hawatambui wala kuona mchango wa Vatican na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wengi, lakini kwa ujumla, Serikali na watu wake wanathamini mchango unaotolewa na Vatican katika mchakato wa kutafuta mafao ya wengi, kwa kuzingatia kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu. Huu ni mchango wa Kanisa unaobubujika kutoka katika imani, uzoefu na mang’amuzi ya Kanisa katika historia ya binadamu.

Askofu mkuu Gallagher anasema kwamba, Marehemu Askofu mkuu Michael Courtney, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi na kuuwawa kikatili ataendelea kuwa ni mfano bora katika maisha na utume wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, mara tu baada ya kifo chake, aliteuliwa kwenda kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi, kunako mwaka 2004. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya kujenga msingi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Askofu mkuu Gallagher anakiri kwamba, katika maisha na utume wake kama Mwanadiplomasia wa Vatican amesaidiwa na watu mbali mbali aliokutana na kufanya nao kazi katika Balozi mbali mbali za Vatican na alipokuwa kwenye Sekretarieti ya Vatican. Hapa amekutana na watu wa kila aina, kila mtu akiwa na malengo, lakini zaidi kwa ajili ya kulitumikia Kanisa. Kuwa mwanadiplomasia wa Vatican si mali kitu, bali Upadre ndio wito ambao mtu anapaswa kujivunia na kuhakikisha kwamba, anautunza na kuuendeleza kwa hali na mali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.