2015-02-02 07:59:32

Vijana chakarikeni, msichague kazi!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Bodi ya Mamlaka ya Vyuo Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini uelekeze jicho lake Nyanda za
Juu Kusini na kuandaa vijana wenye weledi na stadi ya uchimbaji madini
ili kukabili changamoto za soko.

Ametoa wito huo Jumamosi, Januari 31, 2015 wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Songea mjini, mkoani Ruvuma ambako pia alikabidhi vyerehani 20 vyenye thamani ya sh. milioni 4/- kwa wanafunzi 20 waliohitimu kozi ya ushonaji mwaka 2014.


Waziri Mkuu ambaye aliwasili Songea mjini Ijumaa jioni akitokea Dodoma, alifanya kazi hiyo ya kukabidhi vyerehani ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Julai 20, 2013 wakati akizindua chuo hicho alipofanya ziara ya kikazi kwenye mkoa huo. “Katika kipindi kifupi, mkoa wa Ruvuma umeanza kubadilika kwa kasi ya haraka. Kuna madini ya urani, makaa ya mawe na dhahabu. VETA inapaswa iangalie fursa hii kwa kuandaa vijana wenye stadi za uchimbaji madini ili wakati wawekezaji wakianza kuchimba tayari muwe na watu wa kufanya hiyo kazi kutoka kwenye mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu.


“Wasilianeni na Wizara ya Nishati na Madini ili mjue mahitaji yao kwenye eneo hili ni yapi. Wakianza uchimbaji watataka watu wa kufanya kazi hizo. Andaeni vijana... siyo mkae tu na kuja kushtukizwa au mjikute vijana kutoka mbali wanapata hizo ajira wakati wa kwenu wangeweza kunufaika na fursa hii,” alisema.


Aliwataka vijana wanaosoma katika chuo hicho wasome kwa bidii na kuacha kasumba ya kuchagua kazi na kuonea aibu baadhi ya kazi. “Someni, someni sana kwa sababu ustawi wa maisha ya Mtanzania hapo baadaye unategemea elimu ya ufundi. Tuachane na fikra potofu za kuchagua kazi. Kama ni mpishi fanya kazi ya upishi vizuri sababu walaji wapo, hawaishi,” alisisitiza.


Alisema VETA inaweza kuwa suluhisho la ukosefu wa ajira hapa nchini kwa sababu ufundi na stadi wanazopata wahitimu wa vyuo hivi vinapaswa kuwapatia ajira. “Tanzania ina wakazi milioni 45 na wote hawa wanataka kuvaa. Mkianzisha kikundi kidogo kuamua kushona tu sare za shule, tayari mtakuwa mmetoa jibu kwa hitaji la sare za wanafunzi. Wamachinga watanunua kwenu na kuuza lakini na ninyi pia mtapata fedha kuendeshea mradi wenu,” aliwasisitizia wahitimu hao.


Mapema, akisoma risala ya chuo hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Kanda ya Nyanda za Juu, Bw. Kabaka Ndenda alisema chuo hicho kimekwishatoa wahitimu wa kozi fupi 2,627 katika fani mbalimbali za mafunzo ambapo kati yao wavulana ni 2,202 na wasichana ni 425. Aliiomba Serikali iiangalie VETA kisera zaidi kama mkombozi wa ajira hasa wakati huu ambapo vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira. Alizitaja baadhi ya kozi zinatoloewa chuoni kuwa ni mafunzo ya udereva wa magari na pikipiki; uhazili; utengenezaji wa kompyuta; umeme wa jua; umeme wa majumbani; ulimbwende (cosmetology) na upishi.

Alisema chuo hicho kwa sasa kina wanafunzi 298 wanaoendelea na kozi
mbalimbali na mwaka huu kinatarajia kudahili wanafunzi 306.








All the contents on this site are copyrighted ©.