Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe
2 hadi tarehe 8 Februari 2015 limeanza mkutano wake mjini Vatican, utakaokuwa ni fursa
ya kuzungumza na kujadiliana na viongozi mbali mbali wa Sekretarieti ya Vatican, kuhusu
hali ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Viongozi wakuu wa SECAM watapata
pia fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkutano
wao hapa mjini Vatican.
Ujumbe wa viongozi wakuu wa SECAM unaongozwa na Askofu
Gabriel Mbilinyi, Rais wa SECAM. SECAM itapitia tena mikakati ya ushirikiano na Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, hasa zaidi kuhusiana na semina itakayojadili
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, inayotarajiwa kufanyika nchini Msumbiji,
mwezi Mei, 2015.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.