Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo.
Tunanakukaribisha kwa mara nyingine tena tuendelee kukitegea sikio kipindi chetu
cha Kanisa la nyumbani. Kwa vipindi vilivyopita tulitazama familia kama shule ya maadili
na fadhila mbalimbali.
Lengo letu:
tunataka familia zetu na taasisi zote za malezi, ziwe vitalu vya kuandaa watu wema,
watu wenye kufaa kulijenga taifa na Kanisa. Pasipo kuwekeza katika malezi bora kwa
watoto wetu, hapo tujue kwamba tunachangia kwa kiasi kikubwa kuangamia kwa kizazi
kijacho.
Tukichunguza kwa makini kabisa na kwa jicho-wajibifu, tutaona ishara
mbalimbali zinajitokeza ambazo zinaashiria kwa uwazi kabisa uangamizi wa kizazi kijacho.
Ishara hizo ni pamoja na watu kutokujipenda kwa kujiweka daima katika matendo hatarishi;
wazazi kutopenda kuwa jirani na watoto wao, kwa kisingizio cha kazi na utafutaji wa
mali, uadui usioelezeka unaojengeka kati ya watoto na wazazi, watu kuchukiana kwa
viapo na kutopenda kabisa kusameheana, kukua kwa tabia ya kuchukia uhai, kuongezeka
kwa roho mbaya, kukosa kabisa kuthamini utu na badala yake kujali zaidi mali na fedha.
Kuna ongezeko la tabia ya kutokutunza mazingira, kitu ambacho ni urithi wetu
kwa kizazi kijacho; wenye dhamana ya kutoa elimu kwa watoto wetu, kutothamini uadilifu
na ubora wa elimu, jambo ambalo linachangia kuandaa akili-tundu kwa watoto wetu. Mambo
haya na mengine mengi yanayofanana na hayo ni ishara za mchango wetu kwa uangamizi
wa kizazi kijacho.
Tufanye nini basi? Pamoja na kuiangazia familia kama shule
ya maadili, sisi sote tulialikana na tunaendelea kualikana kujibidisha katika majiundo
binafsi, yaani kukomesha kabisa vilema vyetu vya roho na mwili, kujikuza zaidi katika
fadhila, ili sisi wenyewe tuwe watu tunaojifaa na kuwafaa jirani zetu. Katika maisha
yetu ya kila siku kuna wakati huwa tunatambua mapungufu yetu iwe ni kwa kuambiwa au
kwa kujua sisi wenyewe.
Lakini huwa inakuwa vigumu sana kujikubali na kujichukulia
hatua! Tunajiogopa sisi wenyewe hadi tunashindwa kujipatia katazo binafsi, kujiwekea
mkakati mpya wa kuinuka na kusonga mbele. Ndio maana tunabaki katika makosa yaleyale,
vilema vilevile miaka yote. Tunajitesa na kutesa familia, jamaa na majirani kwa vilema
vyetu ambavo kwa kiburi kikavu tu, na uzembe-baridi hatutaki kujikwamua na kujirekebisha.
Jipe moyo, chukua hatua, unaweza kubadilika na kuwa mwema zaidi na zaidi. Amua sasa!!
Pamoja
na majiundo binafsi, tusikose kuliinamishia sikio-zikivu Kanisa Takatifu. Tumsikilize
kwa makini mama Kanisa mtakatifu ambaye daima anatupa miongozo ya utu wema. Dhamiri
zetu ziwe na hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu inatusaidia kutenda yote kwa roho ya uwajibikaji
na kujali mafaa adilifu ya wengi. Pasipokuwa na hofu ya Mungu, daima tutatenda mambo
hatarishi ambayo yatatuangamiza sisi wenyewe na hatimaye kuandaa mazingira na mifumo
angamizi kwa kizazi kijacho. Neno hili litusaidie kujenga dhamiri-wajibifu kwa kizazi
kijacho. Tutambue kwa dhati kwamba, hali yoyote, iwe njema au mbaya kwa kizazi kijacho
hutegemea zaidi mifumo tunayoiweka sisi tunaoishi sasa.
Kwa kuzingatia ukweli
huo ndio maana Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, akitufundisha juu ya dhambi saba
za jamii, alitaja mambo kama uharibifu wa mazingira na maonezi ya kijamii. Kwa uharibifu
wa mazingira tunakidhulimu kizazi kijacho haki ya kuishi katika mazingira bora. Kwa
maonezi ya kijamii, tunaandaa watu wenye hasira, wasiojipenda, wenye chuki kali kwa
wenzao, wenye roho ya kulipiza visasi, wasiojisikia vizuri kuishi duniani hapa.
Tunaahirisha
kipindi chetu cha leo kwa kunidhamishana neno hili: kila mmoja wetu ajiunde hivi ili
awe mtu wa kufaa katika jamii inayomzunguka. Nasi sote kwa pamoja tuone na tuonje
kwa dhati kuwa ni wajibu wetu wa dhati kabisa kuandaa mazingira bora kwa kizazi kijacho.
Kizazi kijacho tunacho tayari mikononi mwetu. Tujiulize daima, tunataka jamii yetu
iwe ya aina gani?
Tusikilizani tena kipindi kijacho!! Kutoka katika studio
za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB