2015-01-31 08:58:40

Ujumbe wa matumaini!


Katika hali ya kuchoka na kukata tamaa baada ya kuvua samaki usiku kucha, Yesu aliwatokea mitume wake akawaambia kushusha nyavu zao, kwa imani na matumaini, Petro akamwambia Yesu, kwa neno lako, tutazishusha nyavu zetu na hapo, wakashangaa kwa wingi wa samaki waliopata.

Huu ndio ujumbe wa matumaini unaotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini baada ya mateso na masumbuko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, sasa wanaitaka Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha: haki, amani, umoja na upatanisho wa kitaifa na kwamba, hakuna tena sababu msingi ya kuhalalisha vita na kwamba, inapaswa kukomeshwa mara moja!

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini, linawaalika viongozi wa kisiasa kuanza kujikita katika majadiliano ya kina, ili kusaidia mchakato wa kupata suluhu ya kudumu, kwa kuthubutu kwenda mbali zaidi, licha ya jitihada ambazo pengine hapo awali hazikuweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, ili kurejesha tena misingi ya haki, amani na utulivu na kwamba, Maaskofu wanapenda kuwaunga mkono kwa jambo hili.

Vita inapaswa kusitishwa mara moja, vinginevyo, Sudan ya Kusini itabaki kuwa ni makaburi tupu na hatimaye kutoweka katika ramani ya dunia kwani vita ni uovu na kinyume cha mapenzi ya Mungu. Watu waoneshe ujasiri wa kusema kwamba, vita ni dhambi bila kupindisha maneno. Vita haiwezi kuwa ni sababu ya majadiliano ya kila siku huko Addis Ababa, wakati watu wanapoteza maisha nchini Sudan ya Kusini. Hakuna ushindi wa kisiasa unaopatikana kwa njia ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, Kanisa kama Mama na Mwalimu, linaomboleza kwa vifo vya watoto wake wote bila ubaguzi.

Chanzo kikubwa cha vita, kinzani na migogoro ya kijamii ni uchu wa mali na madaraka pamoja na tabia ya kutaka kulipizana kisasi, taifa la Sudan ya Kusini linapaswa kuepushwa na majanga kama haya ambayo hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu, wanasiasa watambue kwamba, uongozi ni huduma inayopania kukoleza: haki na amani; maendeleo na ustawi wa raia wake wote kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi.

Mpasuko uliojitokeza Sudan ya Kusini tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2013 ni matokeo ya: rushwa na ufisadi; ukabila na upendeleo; ukosefu wa sera na mikakati madhubuti ya maendeleo; udhaifu katika kurekebisha mfumo wa vikosi vya ulinzi na usalama. Umefika wakati badala yakutumia fedha kununulia silaha, fedha hizo sasa zielekezwe katika ujenzi wa miundo mbinu pamoja na kuimarisha demokrasia ya kweli kwa kutekeleza kwa matendo mkataba wa amani uliofikiwa mjini Arusha, Tanzania mwanzoni mwa mwezi Januari.

Uchaguzi mkuu unaweza kufanyika Juni 2015, lakini utawala wa sheria na Katiba ya nchi ni mambo msingi ya kuzingatiwa, kumbe, kuna haja kwa wadau mbali mbali kushirikiana kwa pamoja katika kipindi hiki cha mpito, hadi mazingira yatakaporuhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Ukwapuaji wa maeneo makubwa ya ardhi, migogoro ya ardhi; kinzani kati ya wakulima na wafugaji ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa kikamilifu, ili kulinda na kudumisha amani na utulivu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linaonya kwamba, kuna idadi kubwa ya silaha za kisasa zinazomilikiwa na raia kinyume cha sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani na usalama wa raia na mali zao. Maaskofu wanawataka wananchi kujikita katika utawala wa sheria. Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini katika mchakato wa kujenga msingi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki linawaaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina na mapana ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani na badala yake, kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo, udugu na umoja kati ya watu, tayari kujikita katika mchakato amani na upatanisho wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linahitimisha ujumbe wake wa matumaini kwa kuwataka wananchi wa Sudan ya Kusini kuachana kabisa na vita na badala yake kushirikiana kwa pamoja katika mchakato wa ujenzi, ustawi na maendeleo ya wananchi wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.