2015-01-31 14:39:50

Kilimo na maadili kwanza!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 31 Januari 2015, amekipongeza Chama cha Wakulima Kitaifa nchini Italia, Coldiretti kwa kuadhimisha miaka 70 tangu kilipoanzishwa, kwa kusema kwamba, ukulima ni kazi ya binadamu na ina umuhimu wake wa pakee, changamoto kwa wakulima ni kuhakikisha kwamba wanatumia vyema ardhi ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakulima wawe waangalifu katika shughuli za kilimo, huku wakijitahidi kuilinda ardhi.

Baba Mtakatifu anasema hakuna ubinadamu pasi na kilimo na wala hakuna maisha bora bila chakula, kinachozalishwa na wakulima kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kumbe kilimo kinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani huu ni wito na wajibu wa binadamu, unaopaswa kuheshimiwa kwa kuwa na sera makini: kisiasa na kiuchumi, kwa kuondoa vikwazo vinavyosababisha vijana wa kizazi kipya kutochangamkia shughuli za kilimo, ingawa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu masomo yao kutoka katika shule za kilimo.

Sekta ya kilimo isaidie Jumuiya ya Kimataifa kutambua na kuona: umaskini na baa la njaa, mambo yanayowanyanyasa watu wengi duniani, ingawa kuna uzalishaji mkubwa wa chakula ambacho kingeweza kutosheleza mahitaji ya watu wengi duniani. Ikumbukwe kwamba, mazao ya nchi yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi, kama wanavyohimiza Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kanuni na sheria tenge katika soko la kimataifa, matumizi mabaya ya mazao ya chakula na hali ya kutowajali jirani ni mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa, kwani yanachangia uwepo wa majanga katika familia nyingi za binadamu. Hapa anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kuangalia kwa makini mchakato wa uzalishaji na ugavi wa mazao ya chakula, ili kuondokana na baa la njaa, kwani chakula hakiwezi kuchezewa ni sehemu ya utakatifu wa maisha ya binadamu na kamwe hakiwezi kuangaliwa kama bidhaa tu.

Wakulima wanaalikwa kulima na kutunza ardhi, ili kuweza kukabiliana kikamilifu na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzalisha chakula bora kwa ajili ya mahitaji ya binadamu, vinginevyo kutakuwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira na madhara katika maisha ya mwanadamu. Hapa Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana kikamilifu ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kulima na kuendelea kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha leo na kile kijacho.

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kuchangamkia shughuli za kilimo, kwa kuanzisha kilimo endelevu kama Mwenyezi Mungu alivyopenda kuikirimia familia ya binadamu; historia ambayo inamwilishwa katika uhalisia wa maisha. Wakulima waongozwe na kanuni maadili ili kazi yao iweze kuzaa matunda kwa ajili ya mafao ya wengi na kama njia ya kupambana na changamoto katika shughuli za uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.