2015-01-30 09:18:06

Maaskofu wakuu kuvikwa Pallio Takatifu Majimboni mwao!


Baba Mtakatifu Francisko amefanya mabadiliko juu ya utaratibu wa Maaskofu wakuu wapya kuvikwa Pallio Takatifu, mabegani mwao, kielelezo cha Yesu Kristo Mchungaji mwema, kwamba, kuanzia tarehe 29 Juni 2015, hawatavikwa tena na Baba Mtakatifu na badala yake, watavikwa na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika.

Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki, Maaskofu wakuu walikuwa wanavikwa Pallio Takatifu katika Ibada ya Misa Takatifu ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Tukio hili sasa litafanyika kwenye Majimbo makuu na kazi hiyo itafanywa na Mabalozi wa Vatican, lengo ni kuhakikisha kwamba, Familia ya Mungu na hususan Maaskofu wa Majimbo mahalia wanaounda Jimbo kuu, wanashiriki kikamilifu katika tukio hili la neema na baraka ya Mungu.

Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia uhusiano uliopo kati ya Maaskofu wakuu ambao wameteuliwa katika kipindi cha mwaka na Makanisa mahalia, ili kutoa nafasi hata kwa waamini katika Majimbo haya kushiriki katika matukio muhimu kama haya ndani ya Kanisa.

Kwa mantiki hii, bado kuna mwendelezo wa umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu wakuu pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati na Kanisa mahalia. Mabadiliko haya yanatajirisha tukio la kuwavika Maaskofu wakuu Pallio Takatifu, kielelezo cha mshikamano wao na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.