2015-01-30 09:42:45

Katekesi na Uinjilishaji ni sawa na uji kwa mgonjwa!


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya anasema, Katekesi na Uinjilishaji mpya ni chanda na pete, kwani ni mambo makuu mawili ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kujikita katika uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayomwilishwa katika imani tendaji! Hii ndiyo njia makini ya waamini kuweza kuwashirikisha jirani, imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Katekesi ya kina haina budi kujikita katika maisha ya kiroho, ili kwamba, mafundisho tanzu ya Kanisa yasaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani; tayari kwa waamini kuweza kushuhudia mahusiano ya kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Haya ni kati ya mambo ambayo yameibuliwa hivi karibuni wakati wa kongamano la siku mbili lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa uinjilishaji mpya na wakuu wa Tume za Katekesi kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya. Wajumbe wamewezesha kushirikishana uzoefu, mang'amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa ufundishaji wa katekesi makini miongoni mwa Watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makatekista kuwa watangazaji na mashuhuda makini wa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Katekesi ni chombo cha Uinjilishaji mpya na kwamba, Katekesi haina budi kuambatana na tasaufi ya maisha ya kiroho; kama inavyofafanuliwa kikamilifu katika Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium. Katekesi haina budi pia kujikita katika mawasiliano ya kina na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, lina zaidi ya Makatekista nusu millioni, wanaojisadaka kila siku kwa ajili ya kuwafundisha na kuwarithisha watoto, imani, maadili na tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.