2015-01-29 07:29:16

Sanaa ya kuhubiri!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha, Evangelii gaudium, anaonesha msisitizo wa pekee katika mahubiri, changamoto ambayo ilikwishawahi kutolewa na Mababa wa Sinodi na hatimaye, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akakazia zaidi katika Nyaraka zake za kitume, Neno la Mungu, Verbum Domini na Sakramenti ya Upendo, Sacramentum caritatis. RealAudioMP3

Huu ni mwendelezo wa changamoto ambazo zilifanyiwa kazi na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa na matokeo yake, Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa limetoa Mwongozo kwa ajili ya mahubiri.

Mwongozo huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza inahusu mahubiri katika Liturujia. Hapa Baraza linafafanua asili na umuhimu wa mahubiri sanjari na mambo msingio yanayoambatana na mahubiri, yaani Mklero aliyewekwa wakfu kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na mwenye dhamana ya kusoma na kulifafanua Neno la Mungu. Ni kiongozi anayepaswa kujiandaa kikamilifu kabla ya kuingia Altareni, ikiwa ni pamoja na kuwatambua waamini au wasikilizaji wake.

Sehemu ya pili ya Mwongozo huu inahusu sanaa ya kuhubiri, inayopembua kwa kina na mapana mbinu na maudhui yanayopaswa kuwasilishwa mbele ya Familia ya Mungu wakati wa mahubiri. Kuna mwongozo wa namna ya kuhubiri katika Jumapili za kawaida, wakati wa Sherehe na Siku kuu, lakini kwa namna ya pekee wakati wa Kipindi cha Juma kuu, Kwaresima, Majilio, Noeli na Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Kuna maelezo ya kina kuhusu mahubiri wakati wa matukio maalum kwa maisha ya waamini, kwa mfano wakati wa kufunga ndoa au mazishi.

Hapa kuna mambo msingi ambayo yanapaswa kugusiwa wakati wa mahubiri kutoka katika Maandiko Matakatifu, Agano la Kale, Agano Jipya na Injili. Hapa mkazo unawekwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu na Liturujia ya Ekaristi pamoja na mpango mzima wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa kuna ujumbe unaogusa Biblia na Ekolojia katika maadhimisho ya fumbo la maisha; kati ya kusikiliza Neno la Mungu pamoja na kuzingatia adhira inayokusudiwa.

Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa, mwishoni, linaweka kiambatanisho kinachoonesha uhusiano uliopo kati ya Mahubiri na Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa kuweka mkazo wa pekee kwa wahubiri kufanya rejea katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Kiambatanisho cha pili kinaonesha baadhi ya nyaraka za Mababa Watakatifu kuhusiana na mahubiri.

Muswada wa mwongozo huu baada ya kufanyiwa tathmini ya kina na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa na hatimaye kupitishwa wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza uliofanyika Mwezi Februari na Mei, 2014, ukapelekwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameagiza kwamba Mwongozo huu uchapwe kwa ajili ya kuwasaidia Wakleri katika kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya mahubiri, yaliyoandaliwa kwa umakini mkubwa, ili kuzima kiu ya udadisi wa kutaka kufahamu undani wa Maandiko Matakatifu.

Ni matumaini ya Baraza kwamba, Mwongozo huu utasaidia waamini kukutana kwa furaha na mwanga wa Roho Mtakatifu kwa njia ya mahubiri, kwa kujikita katika Neno la Mungu na wala si kwa ajili ya kuwafurahisha walimwengu. Mwongozo huu utafanyiwa tafsiri katika lugha mbali mbali, lakini kwa kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.