Yesu ameanzisha njia mpya ambayo wafuasi wake wanapaswa kuifuata kwa kuzingatia kwanza
kabisa kwamba, wanahamasishwa kuwashirikisha na kuwamegea jirani zao imani, matumaini
na mapendo; ili kuepuka kishawishi cha baadhi ya watu kutaka kubinafsisha imani ambayo
ni mlango wa wokovu. Wote wamekombolewa na Yesu, lakini Yesu anamfahamu kila mtu kwa
jina, kwani amemwona, akamtambua na hatimaye, akayamimina maisha yake.
Mwenyezi
Mungu tangu mwanzo amependa kumkomboa mwanadamu kwa njia ya taifa teule, kama alivyofanya
kwa Ibrahim, Baba wa imani, changamoto kwa waamini kusaidiana na kutaabikiana, kwani
kishawishi cha kutaka kubinafsisha wokovu ni njia iliyopotoka. Hii ni sehemu ya mahubiri
yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko
mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 29 Januari 2015.
Baba Mtakatifu anasema, imani
inayojikita kwa Yesu inawasafisha waja wake; matumaini yanawawezesha kupata ahadi
za Mungu na hivyo kuendelea kusonga mbele pasi na kukata tamaa na kwamba, mapendo
yanawawezesha waamini kusaidiana kwa njia ya matendo ya huruma. Kumbe, imani ni zawadi
inayowasukuma waamini kuwashirikisha wengine na wala si jambo la mtu binafsi, bali
inapania wokovu wa wote.
Baba Mtakatifu Francisko anaonya tabia ya baadhi ya
waamini kudhani kwamba wao ni bora zaidi kuliko jirani zao. Jumuiya ya waamini inapoanza
kumeguka katika makundi madogo madogo ni dalili za watu kutaka kubinafsisha wokovu
ambao kimsingi ni zawadi ya wote. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaokoa
watu na wala si tu kikundi cha wateule wachache.
Wakristo wana changamotishwa
kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia kama wamekumbwa na jinamizi la ubinafsi katika
maisha yao ya kiroho au wanajisadaka kwa ajili ya kuwamegea wengine imani, matumaini
na mapendo? Waamini wanaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko kujisikia daima kuwa ni
Taifa la Mungu, ambalo kila mtu amekombolewa na Mwenyezi Mungu anamtambua kwa jina
lake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.