Mh. Padre Jean-Bertin Nadonye Ndongo ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Lolo, DRC
Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung'atuka kutoka madarakani lililowasilishwa
kwake na Askofu Ferdinand Maemba Liwoke wa Jimbo Katoliki Lolo lililoko DRC kadiri
ya Sheria za Kanisa namba 401 Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua
Mheshimiwa Padre Jean-Bertin Nadonye Ndongo wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu
Francisko, kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Lolo. Hadi uteuzi huu, Askofu mteule, alikuwa
anafanya utume wake kwenye Makao makuu ya Shirika mjini Roma.
Askofu mteule
Jean-Bertin Nadonye Ndongo alizaliwa tarehe 24 Machi 1965 huko Botuzu, Jimbo Katoliki
la Molegbe. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi nchini DRC, akaweka
nadhiri za kwanza tarehe 17 Septemba 1989 na nadhiri za daima hapo tarehe 17 Septemba
1992 na hatimaye, kupadrishwa kunako tarehe 2 Agosti 1993.
Tangu wakati huo
amebahatika kutekeleza utume wake wa Kikuhani kama: Paroko Msaidizi, Gombera Msaidizi,
Mlezi wa Wanovisi; Mshauri mkuu wa mkuu wa Kanda ya DRC, Paroko, Mlezi na Gombera;
Msaidizi na baadaye mkuu wa Kanda ya Wakapuchini DRC na Rais wa Baraza la Wakapuchini
Afrika ya Kati na Afrika Magharibi.
Amewahi pia kuwa Rais wa Baraza la Utawala
wa Taasisi ya Mtakatifu Agostin, Kinshasa. Na kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2012 alikuwa
ni Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika, DRC. Kuanzia mwaka 2012 hadi kuteuliwa
kwake alikuwa ni Mwamuzi mkuu wa Wakapuchini, kwenye Makao makuu ya Shirika mjini
Roma.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.