Wakumbatieni watu kwa njia ya upendo wa Mungu, ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika maadhimisho ya Siku ya kumi na
tisa ya Watawa Duniani, yanayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari, sanjari
na maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Kwa mwaka huu, Siku ya Watawa
Duniani, inaadhimishwa sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Italia linawaambia Watawa kwamba, Familia ya Mungu inapenda kuwaona
watawa wakishuhudia kwa maisha na utume wao, wokovu ambao umefunuliwa na Mwenyezi
Mungu kwa Watu wa Mataifa kwa njia ya Yesu Kristo. Watawa wawe na ujasiri wa kusoma
alama za nyakati, ili kuvuka vikwazo vinavyoweza kuwaandama na kukinzana na maisha
pamoja na utume wao. Watembee katika mwanga angavu, huku wakitafuta amani na utulivu
wa ndani. Hii ndiyo siri kubwa ya urembo, inayowatofautisha watu ambao wamejisadaka
na kujiweka wakfu mbele ya Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.
Watawa
wawe na ujasiri wa kuangalia matukio mbali mbali ya maisha, kwa uwazi na uhuru kamili;
kwa kupima na kuchambua mambo, bila kumtenga wala kumbagua mtu, kwani binadamu wote
wanapaswa kukumbatiwa na upendo na huruma ya Mungu inayoshuhudiwa kwa njia ya ushuhuda
wa maisha ya kinabii yanayotolewa na watawa.
Baba Mtakatifu Francisko katika
barua yake kwa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani anasema kwamba, watawa wanapaswa
kuwa kweli ni chemchemi ya furaha kwa wale wanaowazunguka, kwa kutambua kwamba, wao
katika maisha na utume wao, ni kielelezo makini cha Mwenyezi Mungu anayewaokoa watu
wake. Katika maisha, watawa watakumbana na kinzani, mchoko na hata wakati mwingine
kukata au kukatishwa tamaa.
Wamebarikiwa Watawa wanaosaidiana na kutaabikiana,
ili wasije kuanguka na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Waoneshe ari, moyo na ujasiri
wa kutaka kuendelea kumfuasa Yesu Kristo aliyekuwa: mtii, mseja na fukara. Baraza
la Maaskofu Katoliki Italia linaweka matumaini yao makubwa kwa watawa, kwa mchango
wao unaoweza kusaidia kuharakisha mchakato wa mageuzi katika maisha ya Kikristo kwa
kuonesha njia mpya za kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha sanjari
na kupambana na changamoto za maisha zinazojitokeza kwa sasa.
Baba Mtakatifu
anawakumbusha watawa kwamba, anasubiri kuona makali yao, kwa kujenga mazingira yatakayosaidia
kukuza na kudumisha moyo wa sadaka na majitoleo; kwa kukuza udugu na ukarimu hata
katika tofauti zao, ili kuweza kushirikishana upendo unaokoa. Maisha na utume wao
vishuhudie jinsi ambavyo wanajitahidi kupyaisha karama na kuimwilisha katika mazingira
yanayowazunguka, ili jamii iweze kuboreshwa kwa chachu ya Injili. Hii ndiyo neema
ambayo Mama Kanisa anaomba kwa ajili ya watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa
Duniani.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaendelea kukazia kwa namna ya
pekee kabisa umuhimu wa kuzingatia na kuishi useja kama kielelezo cha ushuhuda wa
uaminifu kwa Mungu na Kanisa kama sehemu ya ushiriki wao katika kazi ya ukombozi,
ili kamwe asiwepo mtu anayepotea bila kupata wokovu. Nadhiri za ufukara na utii ni
kielelezo cha ushuhuda dhidi ya ubinafsi unaotawala na kushika hatamu.
Watawa
wajifungamanishe na Kristo katika maisha yao, kwa ajili ya jirani zao, huku wakionesha
unabii, kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kukaribisha tofauti zinazojitokeza ambazo
kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu. Ulimwengu unaonekana kuwa umegawanyika katika
makundi ya wale "wenye nacho na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi", kumbe ni wajibu
wa watawa kushuhudia moyo wa sadaka, ukweli na mapendo yanayojikita katika huduma.
Watawa
katika maisha na utume wao, washuhudie ubinadamu uliopyaishwa kwa njia ya Yesu Kristo,
tayari kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuwaendea maskini na wale wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii; hawa ndio wale waliopotea na kujeruhiwa. Watawa wawasaidie watu
hawa kung'amua utu na heshima yao; kwani wote hawa wanakumbatiwa na upendo wa Mungu
unaojionesha kwa njia ya upendo unaobubujika kutoka ndani ya Kanisa.
Familia
ya Mungu inakumbushwa kwamba, Mwaka wa Watawa ni kwa ajili ya waamini wote na wala
si kwa watawa peke yao. Waamini wachukue fursa hii pia kufanya toba na wongofu wa
ndani, tayari kupokea na kutumia neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika
maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Waamini walei waoneshe umoja na uwajibikaji
katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia linawatakia kheri na baraka watawa wote katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa
Duniani, waendelee kuonesha jeuri ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo
na Kanisa lake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.